Kan'ani: Israe haina ubavu wala uthubutu wa kuikabili Iran kijeshi
-
Nasser Kan'ani
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema utawala wa Kizayuni wa Israel hauna ubavu wala ujasiri wa kuingia katika makabiliano ya kijeshi na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Nasser Kan'ani Chafi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema hayo jana usiku katika mahojiano na televisheni ya Al-Alam na kuongeza kuwa: Vitisho vilivyotolewa hivi karibuni na utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran ni vita tu vya kisaikolojia.
Amesisitiza kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel hauna ubavu, uwezo wala uthubutu wa kuishambulia kijeshi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Kan'ani amesema bayana kuwa, jibu la Iran kwa hatua yoyote ya kipumbavu ya utawala huo bandia litakuwa kali na la kuumiza.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameashiria safari ya Rais Joe Biden wa Marekani katika eneo hili la Asia Magharibi na kubainisha kuwa, ziara ya Biden haijakuwa na tija yoyote kwani ameshindwa kuunda muungano wa kijeshi dhidi ya Iran kama alivyokusudia. Kan'ani Chafi ameongeza kuwa, nchi za eneo hili haziiamini tena Washigton.
Kuhusu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, Kan'ani amesema Marekani inapaswa kukubali masharti yote ya Iran kwa mujibu wa mapatano hayo ya kimataifa ya mwaka 2015, na kwamba kurefusha mazungumzo ya kujaribu kuhuisha makubaliano hayo hakuna maslahi kwa upande wowote hususan Wamarekani.