Jenerali Baqeri: Vikosi vya Iran vimekuwa na nafasi kubwa kusambaratisha vikwazo
Kamanda Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Iran amesema vikosi vya ulinzi na usalama vya Jamhuri ya Kiislamu vimekuwa na nafasi muhimu katika kuvunja nguzo za kampeni ya maadui ya mashinikizo ya kiwango cha juu dhidi ya taifa hili.
Meja Jenerali Mohammad Hossein Baqeri ameyasema hayo leo Alkhamisi akihutubia makamanda wa Jeshi la Nchi Kavu la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Mashhad, kaskazini mwa Iran na kueleza kuwa, kufeli njama za kibeberu za Marekani katika eneo la Asia Magharibi kunaonesha kuwa dunia inaingia katika marhala mpya inayojulikana kama 'kipindi cha mpito.'
Jenerali Baqeri amefafanua zaidi kwa kusema: Kudhoofu nguvu za Marekani, kusambaratika njama za Washingon katika eneo la Asia Magharibi licha ya kutumia mabilioni ya dola, kuimarika tena nguvu za China na kuondoka Russia katika kipindi cha kukaa kimya, kunadhihirisha wazi kuwa dunia inaingia katika kipindi kipya.
Mkuu huyo wa Kamandi ya Majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, kutokana na uongozi wa kipekee wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, kuwa macho taifa la Iran, na utayarifu wa majeshi ya nchi hii, Jamhuri ya Kiislamu imefanikiwa kustawi na kupata mafanikio mengi licha vita, ukosefu wa uthabiti na usalama na migogoro mingi iliyoshuhudiwa katika eneo hili katika miaka ya hivi karibuni.
Meja Jenerali Mohammad Hossein Baqeri ameongeza kwa kusema, "Huku Iran ikiingia katika kipindi cha kuchanua fursa mkabala wa vitisho, nguzo za jengo la mashinikizo ya kiwango cha juu zaidi ya maadui zimeporomoka moja baada ya nyingine, na nafasi ya vikosi vya ulinzi katika kufanikiwa hayo ni muhimu sana."