Kuendelea hatua haribifu za Saudia katika soko la mafuta
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i8656-kuendelea_hatua_haribifu_za_saudia_katika_soko_la_mafuta
Katika kuendeleza ushindani wake dhidi ya Iran kuhusiana na mgao wa kila nchi katika soko la mafuta, Saudi Arabia imeshusha bei ya mafuta yake mepesi inayouza kwa nchi za Ulaya.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 07, 2016 02:16 UTC
  • Kuendelea hatua haribifu za Saudia katika soko la mafuta

Katika kuendeleza ushindani wake dhidi ya Iran kuhusiana na mgao wa kila nchi katika soko la mafuta, Saudi Arabia imeshusha bei ya mafuta yake mepesi inayouza kwa nchi za Ulaya.

Kwa mujibu wa gazeti la Wall Street Journal linalochapishwa nchini Marekani, Saudia imechukua hatua hiyo kama jibu na radiamali baada ya kushindwa kufikia malengo yake kuhusu uainishaji kiwango cha uzalishaji mafuta katika kikao cha wiki iliyopita mjini Vienna, cha Nchi Zinazozalisha Mafuta kwa Wingi Duniani (OPEC).

Wall Street Journal limeripoti kuwa shirika la taifa la mafuta na gesi asilia la Saudia ARAMCO limewaandikia washitiri wake baruapepe na kutangaza kuwa limepunguza bei ya mafuta yake mepesi kwa senti 35 kwa nchi za kaskazini magharibi mwa Ulaya, na senti 10 kwa nchi za eneo la Mediterania katika shehena litakayosafirisha kuanzia mwezi ujao wa Julai.

Punguzo hilo la bei la mafuta ni la kustaajabisha, kwa sababu kutokana na kumalizika awamu ya kufanyiwa matengenezo na masawazisho viwanda vya kusafisha mafuta, mahitaji ya ununuzi wa mafuta huwa yanaongezeka katika nusu ya pili ya mwaka.

Hatua hiyo ya Saudia imechukuliwa katika hali ambayo Iran ilianza kuuza mafuta yake kwa nchi za Ulaya tangu mwezi Februari baada ya kuondolewa vikwazo vya mafuta vya Umoja wa Ulaya. Hivi sasa uuzaji mafuta wa Iran kwa nchi za Ulaya umefikia kiwango cha mapipa laki nne kwa siku. Kwa mujibu wa maafisa wa Iran, baada ya makubaliano yaliyofikiwa kati ya Tehran na viwanda vya kusafisha mafuta vya Ugiriki, Ufaransa na Italia, kiwango hicho katika kipindi cha miezi ijayo kitafikia mapipa laki saba kwa siku.

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Kimataifa la Nishati uuzaji wa mafuta ya Saudia kwa nchi za Ulaya katika mwaka uliopita ulikuwa mapipa laki nane kwa siku.

Hadi sasa utawala wa Riyadh umekuwa ukifanya kila njia kupitia uuzaji mafuta yake kwa bei rahisi ili kuizuia Iran isiweze kurejea tena kwenye masoko ya mafuta.

Alipozungumza wiki iliyopita na waandishi wa habari katika kikao cha mawaziri wa mafuta na nishati wa nchi wanachama wa OPEC huko mjini Vienna, Waziri wa Nishati wa Iran Bijan Namdar Zanganeh, alitangaza kuwa lengo la Iran ni kuzalisha mapipa milioni nne ya mafuta kwa siku hadi ifikapo mwishoni mwa mwaka huu. Akiashiria mgao wa asilimia 14.5 wa kuzalisha mafuta katika OPEC ambao Iran ilikuwa nao kabla ya kuanza kuwekewa vikwazo, Zanganeh alibainisha kuwa hivi sasa Iran inazalisha zaidi ya mapipa milioni tatu na laki 800 kwa siku. Alifafanua kuwa kuna baadhi ya watu ambao hawakuamini jambo hilo, lakini ukweli ni kwamba Tehran imeweza kuongeza zaidi kasi ya uzalishaji wake kuliko ilivyokuwa imekadiriwa na itaendelea kuongeza kiwango cha uzalishaji hadi itakapopata tena mgao wake halisi katika soko la mafuta.

Saudia, ambayo kutokana na kuporomoka bei ya mafuta imekabiliwa na nakisi ya bajeti ya dola bilioni 100, hivi sasa inataka kuuza hisa za shirika lake la mafuta la Aramco.

Katika kipindi cha juma hili, bei ya mafuta ya OPEC ilifikia dola 44 na senti 65 kwa pipa ikiwa ni ongezeko la senti 11 kulinganisha na wiki ya kabla yake. Katika kikao cha wiki iliyopita cha OPEC Saudia ilishikilia kuainishwe mgao wa kiwango cha uzalishaji baina ya nchi wanachama ili kuandaa mazingira ya kuongezeka bei ya mafuta lakini haikufanikiwa kufikia lengo lake hilo. Ukweli ni kwamba Riyadh haiwezi kuzishawishi nchi nyengine wanachama wa OPEC zipunguze uzalishaji wao, wakati yenyewe inazalisha mafuta zaidi ya mgao wake na kuyapeleka masokoni. Kutokana na sera za Saudia, ni jambo lisilo na maana yoyote kuziainishia nchi nyengine mgao wa kiwango maalumu cha uzalishaji.

Katika mazingira kama haya huenda ikaonekana jambo gumu kutabiri mabadiliko yatakayojiri katika soko la mafuta, lakini kwa uchache tunaweza kusema kuwa nafasi ya Saudia katika masoko ya mafuta inaendelea kudhoofika na haihitaji utaalamu mkubwa kutabiri hali ngumu zaidi itakayoukabili uchumi wa kutegemea mafuta wa Saudia katika siku za usoni.../