Jeshi la Iran laendeleza mazoezi ya ndege za kivita zisizo na rubani
(last modified Thu, 25 Aug 2022 08:05:42 GMT )
Aug 25, 2022 08:05 UTC
  • Jeshi la Iran laendeleza mazoezi ya ndege za kivita zisizo na rubani

Mazoezi ya Pamoja ya Ndege Zisizo na Rubani (droni) 1401 ya Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yameendelea kwa siku ya pili leo ambapo droni za kivita zimefanikiwa kutekeleza oparesheni zao kwa mafanikio.

Mazoezi hayo ambayo yalianza Jumatano yanajumuisha droni za kivita 150 na yanafanyika kote katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Katika mazoezi hayo ya siku mbili ndege za kivita zisizo na rubani zinafanya mazoezi kuanzia eneo la kusini mwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman hadi maeneo ya masharik, magharibi, kaskazini na kati mwa nchi.

Akizungumza kabla ya kuanza mazoezi hayo jana, Admeri Habibollah Sayyari, Naibu Mratibu wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameeleza kuwa, matawi yote manne ya jeshi la Iran yameshirikishwa kwenye mazoezi hayo ya kijeshi.

Admeri Sayyari amebainisha kuwa, maneva hayo yamefanyika sambamba na kuanza Wiki ya Kitaifa ya Serikali hapa nchini, na yatafanyika katika pembe zote za Jamhuri ya Kiislamu.

Ofisa huyo mwandamizi wa jeshi la Iran ameongeza kuwa, droni 150 zilizozalishwa na wataalamu wa Iran wakishirikiana na mashirika ya wanataaluma ya hapa nchini zitarushwa na kufanyiwa majaribio katika luteka hiyo.

Ndege ya kivita isiyo na rubani ya Jeshi la Iran katika mazoezi

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hivi sasa ni moja ya nchi chache duniani ambazo zinaendelea kupiga hatua mbele katika ubunifu, upanuzi na uundaji wa aina tofauti za ndege zisizo na rubani.

Brigedia Jenerali Amir Ali Hajizadeh, Kamanda wa Kikosi cha Anga za Mbali cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC alisema hivi karibuni kuwa: "huko nyuma, sisi hatukuwa na uwezo tulionao leo hii, na hivi sasa tunauza nje ya nchi makombora na ndege zisizo na rubani."

Tags