Iran yamkosoa Biden kwa kuunga mkono, kushajiisha ghasia hapa nchini
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imelaani vikali hatua ya Marekani ya kuingilia masuala ya ndani ya Jamhuri ya Kiislamu, baada ya Rais Joe Biden wa nchi hiyo kutangaza kuwa anaunga mkono ghasia na fujo zinazoshuhudia hapa nchini.
Nasser Kan’ani Chafi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema katika taarifa leo Jumamosi kuwa, Biden kwa mara nyingine tena ameingilia masuala ya ndani ya nchi hii, kwa kutangaza kuunga mkono na kushajiisha ghasia hapa nchini.
Amesema, "Kwa kuzingatia ukweli kwamba (Biden) hana washauri wa kuaminika au kumbukumbu nzuri, namkumbusha kuwa Iran ni (taifa) imara na lenye nguvu, na haliwezi kusalimu amri kwa vikwazo vyake vya kikatili na vitisho."
Kan'ani Chafi ameeleza kuwa, taifa la Iran lenye fahari, kamwe haliwezi kubabaishwa na matamshi ya uingiliaji ya mwanasiasa mkongwe, ambaye amekuwa akiendesha kwa muda mrefu bila mafanikio, kampeni dhidi ya Wairani.
Biden hapo jana alibwabwaja kwa kusema "ameshangazwa na ujasiri wa watu wanaomiminika mabarabarani kuandamana nchini Iran."
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameashiria mfumo wa siasa za Marekani ulivyojengeka katika misingi ya uingiliaji na mauaji na kusisitiza kuwa: Tangu mapinduzi ya 1953 hadi sasa, sera za utawala wa Marekani dhidi ya Iran zimenakiliwa vyema katika fikra zetu, na bila shaka, historia na kila sehemu ya dunia itashuhudia juu ya makovu yaliyosababishwa na jinai na ghasia za Marekani.
Hapo jana, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alisema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ndio nanga ya uthabiti na usalama katika eneo la Asia Magharibi, na wala si ardhi ya mapinduzi.
Hossein Amir-Abdollahian alisema hayo katika mazungumzo yake ya simu na Josep Borrell, Mkuu wa Sera za Kigeni na Usalama wa Umoja wa Ulaya na kusisitiza kuwa, kifo cha Mahsa Amini kimetutia uchungu sisi sote, hata hivyo suala hilo linatumia kama kisingizio na Wamagharibi cha kuingilia masuala ya ndani ya nchi hii.