Amir-Abdollahian: Iran inapinga vikali vita na kuzipatia silaha pande mbili zinazopigana
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: Jamhuri ya Kiislamu inapinga vikali vita na kuupatia silaha upande wowote kati ya pande mbili zinazopigana.
Shirika la habari la IRNA limeripoti kuwa, katika mazungumzo yaliyofanywa kwa njia ya simu kati ya waziri wa mambo ya nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian na waziri wa mambo ya nje wa Croatia anayehusika pia na masuala ya Ulaya Gordan Grlić-Radman, wanadiplomasia hao wakuu wa nchi mbili wamebadilishana mawazo juu ya uhusiano wa pande mbili, wa kikanda na kimataifa na kutilia mkazo kuimarishwa zaidi mashirikiano kati ya Tehran na Zagreb.
Katika mazungumzo yake na Grlić-Radman, Amir-Abdollahian amegusia matukio ya karibuni nchini Ukraine na madai yaliyotolewa na baadhi ya maafisa wa nchi hiyo kwamba ndege zisizo na rubani za Iran ambazo ilipatiwa Russia tokea miaka kadhaa nyuma zimetumika katika vita dhidi ya Ukraine na akasema: "sisi tunapinga vikali vita na kuupatia silaha upande wowote kati ya pande mbili zinazopigana, na tumewaeleza viongozi wa Ukraine kwamba kama wana ushahidi wowote kuhusiana na kutumiwa ndege zisizo na rubani za Iran katika vita dhidi ya nchi hiyo, waonyeshe".
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amebainisha kuwa, "kwa miaka kadhaa Iran ina uhusiano wa kiulinzi na Russia, lakini hatujaunga mkono vita dhidi ya Ukraine na wala hatujaipatia Russia silaha yoyote ya Kiirani ili iitumie katika vita dhidi ya Ukraine".
Katika mazungumzo hayo ya simu, waziri wa mambo ya nje wa Croatia Gordan Grlić-Radman ameashiria maelewano mazuri yaliyopo katika uhusiano kati ya nchi mbili; na mbali na kutilia mkazo msimamo wa nchi yake wa kuunga mkono kufufuliwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA amesema, ataiwasilisha misimamo ya Iran kwa mawaziri wenzake katika Umoja wa Ulaya.../