Iran: Hatutaipatia Marekani fursa yoyote ya ziada katika mazungumzo ya uondoaji vikwazo
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema, Iran inachukua hatua kwa kutumia mantiki na kuchunga mistari myekundu ya Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na haitapatia Marekani fursa yoyote ya ziada katika mazungumzo ya uondoaji vikwazo.
Hossein Amir-Abdollahian ameyasema hayo leo mjini Yerevan, Armenia katika mkutano na waandishi wa habari alipokuwa akizungumzia mchakato wa mazungumzo ya uondoaji vikwazo vya kidhalimu ilivyowekewa Iran kufuatia matamshi yaliyotolewa na maafisa wa Marekani walioeleza kwamba kwa sasa hakuna tena ajenda ya mazungumzo ya uondoaji vikwazo.
Amir- Abdollahian amebainisha kuwa, kuna mgongano katika kauli na mwenendo wa Wamarekani, kwa sababu siku tatu zilizopita ulipokewa ujumbe wa salamu kutoka upande wa Marekani; na Iran ikatangaza kwamba masuala yanayohusu tuhuma zilizotolewa na Wakala wa Atomiki IAEA inapasa yapatiwe ufumbuzi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Wamarekani wanatumia kila njia ili kuyapigia upatu matukio yaliyojiri siku zilizopita nchini Iran na wakati huohuo kutoa mashinikizo ya kisiasa na kisaikolojia ili ijipatie fursa zaidi za kimaslahi katika mazungumzo, lakini akasisitiza kwa kusema: Hakutatolewa fursa yoyote ya ziada kwa Marekani katika mazungumzo yoyote yale.
Katika mazungumzo hayo na waandishi wa habari aliyofanya pamoja na mwenyeji wake waziri wa mambo ya nje wa Armenia, Amir-Abdollahian ameashiria pia kuongezeka kwa mashirikiano ya kibiashara baina ya Iran na Armenia na akasema: limewekwa lengo la kuongezwa kiwango cha mabadilishano ya kibiashara hadi kufikia dola bilioni tatu.
Katika safari yake ya siku tatu nchini Armenia, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa nchi hiyo Nikol Pashinyan, Waziri wa Mambo ya Nje Ararat Mirzoyan na Spika wa Bunge Alen Simonyan juuu ya masuala muhimu zaidi ya pande mbili na ya kimataifa.../