SEPAH: Wananchi wa Iran daima wamekuwa wakiifedhehesha Marekani
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) amesisitiza kuwa, kwa kujitokeza kwao vilivyo katika kuyalinda Mapinduzi ya Kiislamu; muda wote wananchi wa Iran wamekuwa wakiidhalilisha na kuifedhehesha Marekani na kuthibitisha kivitendo matamshi ya Imam Khomeini MA kuwa Marekani haiwezi kulifanyia taifa la Iran upuuzi wowote.
Brigedia Jenerali Hossein Salami amesema hayo katika maziko ya watu waliouawa kwenye shambulio la kigaidi la Haram Tukufu ya Shah Cheragh ya mjini Shiraz, kusini magharibi mwa Iran na kuongeza kuwa, Mapinduzi matukufu ya Kiislamu hayawezi kutetereshwa na vitimbakwiri wachache waliolaghaiwa na maadui.
Shirika la habari la Iran Press limeripoti habari hiyo na kunukuu matamshi ya Kamanda Mkuu huyo wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH akisema kuwa, kujitokeza kwa wingi mno wananchi wa Shiraz katika maziko ya wahanga wa shambulio la kigaidi la haram ya Shah Cheraqh ni ushahidi wa kufeli vibaya maadui wenye chuki kubwa mno na taifa la Iran.
Amesema, kujitokeza kwa wingi wananchi wa Iran waliopevuka kifikra na wenye muono wa mbali katika maziko hayo kumeshindilia msumari wa mwisho kenye jeneza la Marekani, Israel na maadui wengine woga na dhalili.
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) pia amesema, machafuko ya hivi karibuni ya nchini Iran yamechochewa na utawala wa Kizayuni wa Israel na kusisitiza kuwa, maadui hao wamehamaki kutokana na kushindwa vibaya na taifa la Iran katika kipindi cha miaka 43 iliyopita.
Pia amesema, Marekani mtenda jinai, utawala wa Kizayuni na ukoo wa Aal Saud wameona jinsi siasa zao chafu zinavyofelishwa na ushawishi na nguvu za kisiasa na kimaanawi za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hata katika maeneo ya mbali na bila ya shaka wanajua kuwa hawawezi kukabiliana na taifa la Iran.