Jan 01, 2023 03:09 UTC
  • Abdollahian: Iran inapinga uwepo wa madola ajinabi katika eneo

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Tehran inapinga vikali uwepo wa madola ajinabi katika eneo hili la kistratejia la Asia Magharibi.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alisema hayo jana katika mazungumzo ya simu na mwenzake wa Azerbaijan, Jeyhun Bayramov na kuongeza kuwa, mielekeo chanya inaweza kutatua matatizo ya eneo hilo pasi na kuwahitaji maajinabi.

Amir-Abdollahian amebainisha kuwa, uwepo wa maajinabi katika eneo hili la Asia Magharibi (Mashariki ya Kati) katu haujawa na tija nyingine ghairi ya kushadidisha matatizo mbalimbali. Mwandiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran amependekeza kuunda makundi ya pamoja ya wanahabari kujadili uhaba wa maji na uchafuzi wa Mto Aras, ambao unaunda asilimia kubwa ya mpaka wa Iran-Azerbaijan.

Katika mazungumzo hayo, Jeyhun Bayramov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Azerbaijan na Hossein Amir-Abdollahian wamefanya mashauriano kuhusu matukio ya kimataifa, kieneo na kuhusu uhusiano wa pande mbili. 

Manowari ya kijeshi ya Australia katika Ghuba ya Uajemi

Kwa upande wake, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Azerbaijan, Azerbaijan, Jeyhun Bayramov sanjari na kusisitizia haja ya kuimarishwa uhusiano na ushirikiano wa pande mbili wa nchi yake na Iran ameeleza kuwa, msimamo wa Baku wa kufanya juhudi za kuhakikisha kuwa eneo la Mashariki ya Kati linakuwa na amani haujabadilika. 

Amesema serikali ya Azerbaijan ina hamu ya kufanya mkutano wa kamisheni ya pamoja ya uchumi mapema mwaka huu ulioanza wa 2023 Miladia, kwa shabaha ya kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara baina ya mataifa haya mawili jirani.

Tags