Uingereza imekasirishwa na kushindwa kijasusi nchini Iran
Ebrahim Azizi, naibu mwenyekiti wa Kamati ya Usalama wa Kitaifa na Sera ya Kigeni katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema Uingereza kimsingi haisikitishwi na kunyongwa kwa Alireza Akbari kwani daima hutoa kafara kufikia malengo yake ya kijasusi na kwamba kilichoikasirisha Uingereza ni kushindwa katika njama zake za kijasusi,"
Azizi amesema kuwa Akbari alipatikana na hatia ya njama dhidi ya taifa na kuhatarisha sekta ya ulinzi na usalama.
Aidha amesema majasusi kote duniani hushughulikiwa kwa ukali kabisa na huu ni ukweli unaotambulika kimataifa.
Azizi amesema kinachowakera Waingereza ni ukweli kwamba wamegundua kuwa walikuwa wakifanya maamuzi kwa kuzingatia taarifa zisizo sahihi walizopewa na idara za kijasusi za Iran muda wote.
Aliongeza kuwa, "waliwekeza kwa mtu (Akbari) kwa miaka mingi, na sasa wamegundua kuwa idara za usalama za Iran zilikuwa zinamfuatilia kwa karibu, na hilo limewakasirisha."
Aidha amesema hakuna ulazima wa kujibu kauli "zisizo na msingi, wala mantiki" kuhusu kunyongwa kwa Akbari.
Akbari alikamatwa mwaka wa 2019 ambapo alikuwa amepokea euro 1,805,000, pauni 265,000 na dola 50,000 kwa ajili ya kufanya ujasusi nchini Iran kwa niaba ya serikali ya Uingereza.
Mahakama ya Iran imesema Akbari alihukumiwa kifo baada ya kupatikana na hatia ya kueneza "ufisadi katika ardhi" na "shughuli pana dhidi ya usalama wa ndani na wa kimataifa wa nchi" kwa kufanya ujasusi kwa niaba ya shirika la kijasusi la serikali ya Uingereza. Akbari alinyongwa mapema Jumamosi.
Katika taarifa yake siku ya Jumatano, Wizara ya Usalama ya Iran ilimtaja Akbari kama "mmoja wa mawakala waliojipenyeza zaidi wa huduma ya kijasusi ya Uingereza ambapo aliweza kupenya katika vituo nyeti na vya kistratijia vya nchi."
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza James Cleverly alitoa wito wa kuachiliwa kwa jasusi huyo wakati ripoti za mpango wa kumnyongwa zilipoibuka mapema, akisema katika ujumbe wake wa Twitter, "Iran lazima isitishe hukumu ya kunyongwa kwa Alireza Akbari aliyekuwa na uraia pacha wa Iran na Uingereza.
Uingereza ina historia ndefu ya shughuli za kijasusi nchini Iran ambayo inaweza kufuatiliwa tangu mapinduzi ya 1953 dhidi ya serikali iliyochaguliwa kidemokrasia ya Mohammad Mosaddeq.
Vikosi vya kijasusi vya Iran vimewatia mbaroni majasusi wengi wenye uhusiano na mataifa ya kigeni ambao walihusika katika vitendo vya hujuma dhidi ya watu na vituo vya Iran katika miongo kadhaa iliyopita.
Serikali ya Uingereza pia ilihusika kikamilifu katika kuchochea ghasia za hivi majuzi zilizoungwa mkono na madola hasimu ya kigeni nchini Iran baada ya kifo cha mwanamke kijana mwenye asili ya Kikurdi.