Iran yaongeza mauzo ya mafuta na gesi licha ya vikwazo
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i92972-iran_yaongeza_mauzo_ya_mafuta_na_gesi_licha_ya_vikwazo
Shirika la Taifa la Mafuta la Iran (NIOC) limesema kwa wastani katika robo ya kwanza ya mwaka wa Kiirani unaomalizika Machi 20, Iran imekuwa ikiuza bidhaa za mafuta ghafi ya petroli na gesi zenye thamani ya dola milioni 154 kwa siku.
(last modified 2026-08-02T13:18:47+00:00 )
Jan 16, 2023 23:36 UTC
  • Iran yaongeza mauzo ya mafuta na gesi licha ya vikwazo

Shirika la Taifa la Mafuta la Iran (NIOC) limesema kwa wastani katika robo ya kwanza ya mwaka wa Kiirani unaomalizika Machi 20, Iran imekuwa ikiuza bidhaa za mafuta ghafi ya petroli na gesi zenye thamani ya dola milioni 154 kwa siku.

Taarifa hiyo imesema "tukichukulia kuwa pipa moja la mafuta ghafi ni dola 80, kiasi hiki cha mapato ni sawa na mauzo ya nje ya mapipa milioni 1.92 ya mafuta kwa siku.

Kwa mujibu wa takwimu za forodha, jumla ya mapato ya Iran kutokana na mauzo ya gesi ya mafuta ya petroli katika miezi tisa ya 2022 pia yalifikia dola bilioni 6.8, ikiwa ni ongezeko la hadi 86% ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita.

Shirika la habari la Fars liliripoti wiki iliyopita kwamba rasimu ya bajeti ya serikali ya Iran inakadiria kuwa usafirishaji wa mafuta utakuwa mapipa milioni 1.4 kwa siku.

Siku ya Jumapili, shirika la habari la Reuters lilisema mauzo ya mafuta ya Iran yalipanda kiwango kipya katika miezi miwili iliyopita ya 2022 na nchi hii inaanza mauzo yake  kwa nguvu mwaka huu wa  2023 licha ya vikwazo vya Marekani.

Meli iliyosheheni gesi ya LPG

Kufuatia hatua ya Donald Trump kuiondoa Marekani katika makubaliano ya nyuklia ya Iran na kuiwekea tena Iran  vikwazo, mauzo ya nje ya mafuta ghafi ya petroli ya Iran yalishuka hadi kiwango cha mapipa 100,000 kwa siku mwaka 2020 kutoka zaidi ya mapipa milioni 2.5 kwa siku kabla ya vikwazo kuondolewa mwaka 2018.

Mauzo ya nje yameongezeka katika kipindi cha Rais Ebrahim Raisi, na yamefikia kiwango cha juu zaidi tangu 2019 kwa baadhi ya makadirio. Haya yanajiri licha ya kuwepo kwa misukosuko kama vile kukwama kwa mazungumzo ya nyuklia na ushindani kutoka mafuta ghafi ya Russia yaliyopunguzwa bei.

Sara Vakhshouri mshauri wa Nishati wa SVB International, aliyenukuliwa na Reuters, alisema mauzo ya nje ya Iran mnamo Desemba yalikuwa wastani wa mapipa milioni 1.137 kwa siku.