Mwakilishi wa Iran UN akanusha kukutana na mwakilishi wa Marekani
Ofisi ya Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa imekanusha uvumi ulioenezwa na baadhi ya vyombo vya habari kwamba mwakilishi wa Iran katika umoja huo ameonana na mwakilishi maalumu wa Marekani katika masuala ya Iran.
Baadhi ya vyombo vya habari vimeeneza uvumi kuwa, Amir Saeid Jalil Iravani, Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa ameonana na Robert Malley, mwakilishi maalumu ya serikali ya Marekani katika masuala ya Iran.
Katika uvumi wao huo, vyomo hivyo vya habari vimedai kuwa, mwakilishi wa Iran ameonana kwa uchache mara tatu na mwakilishi huyo wa Marekani anayehusika na masuala ya Iran.
Katika upande mwingine, vyombo hivyo vya habari vimemnukuu Ned Price, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani akisema kuwa, hivi sasa kuna mabadilishano ya ujumbe baina ya Washington na Tehran ijapokuwa suala la kufufuliwa mapatano ya nyuklia ya JCPOA halimo kwenye ajenda.
Shirika la habari la Iran Press limeinukuu Ofisi ya Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa ikikanusha uvumi kuwa mwakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu Amir Saeid Iravani ameonana na mwakilishi maalumu wa Marekani kuhhusu Iran, Robert Malley na kusisitiza kuwa, balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa huwa anaonana na watu mbalimbali muhimu wa kisiasa na vyuo vikuu lakini hajafanya mazungumzo na viongozi wa Marekani.