Iran: EU imefanya kosa kubwa kuiweka IRGC katika orodha ya ugaidi
(last modified Thu, 19 Jan 2023 10:38:45 GMT )
Jan 19, 2023 10:38 UTC
  • Iran: EU imefanya kosa kubwa kuiweka IRGC katika orodha ya ugaidi

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Bunge la Ulaya limefanya kosa kubwa kwa kupiga kura ya kuutaka Umoja wa Ulaya na nchi wanachama wa EU kuliweka Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) katika orodha ya makundi ya kigaidi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Hossein Amir-Abdollahian amesema hayo kati mazungumzo yake ya simu na Josep Borrell, Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya (EU) na kuongeza kuwa, Ulaya 'imejipiga risasi mguuni' kwa kuiweka IRGC katika jalada lake la makundi ya kigaidi.

Amir-Abdollahian amekosoa vikali hatua hiyo ya Bunge la Ulaya aliyoitaja kuwa ya kihisia, ghalati, isiyo na hekima, na isiyo ya kitaalamu. Amesema kitendo hicho kinakinzana na mantiki ya siasa na heshima, na kwamba huenda kikawa na matokeo mabaya.

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran amebainisha kuwa, kuna haja ya kuheshimu mifumo ya ulinzi na usalama katika ulimwengu wa diplomasia na kuimarisha hali ya kuaminiana, badala ya kutumia lugha ya vitisho na kuchukua hatua zisizo rafiki.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameeleza kuwa, daima Jamhuri ya Kiislamu imekuwa ikitangaza bayana kuwa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ni taasisi rasmi ya serikali, na ambayo imekuwa na inaendelea kuwa na nafasi muhimu katika kudhamini usalama wa Iran na eneo, haswa katika vita dhidi ya ugaidi.

Wanajeshi wa SEPAH

SEPAH imekuwa ikisisitiza kuwa, muda wote wananchi wa Iran wamekuwa wakiidhalilisha na kuifedhehesha Marekani na maadui wa taifa hili, ambao siku zote wanahamaki kutokana na kushindwa vibaya na taifa la Iran katika kipindi cha miaka 43 iliyopita.

Amir-Abdollahian amesema Bunge la Iran litatoa jibu la nguvu na la kisheria kwa kitendo hicho cha Bunge la Ulaya cha kupiga kura ya kuitaka EU kuliweka Jeshi la SEPAH ya Iran katika orodha ya makundi ya kigaidi. 

Tags