Rais Raisi: Mtazamo wa kumwona mwanamke kama wenzo na bidhaa utashindwa tu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i93092-rais_raisi_mtazamo_wa_kumwona_mwanamke_kama_wenzo_na_bidhaa_utashindwa_tu
Rais Ebrahim Raisi amesema haipasi mwanamke kuwa mtu wa pembeni au kutengwa katika jamii na akasisitiza kuwa mitazamo yote miwili, wa fikra mgando kuhusiana na mwanamke na wa madola na wanasiasa wa Magharibi wa kumwangalia mwanamke kama wenzo tu inaelekea kushindwa na kukataliwa.
(last modified 2026-08-02T13:18:47+00:00 )
Jan 20, 2023 04:31 UTC
  • Rais Raisi: Mtazamo wa kumwona mwanamke kama wenzo na bidhaa utashindwa tu

Rais Ebrahim Raisi amesema haipasi mwanamke kuwa mtu wa pembeni au kutengwa katika jamii na akasisitiza kuwa mitazamo yote miwili, wa fikra mgando kuhusiana na mwanamke na wa madola na wanasiasa wa Magharibi wa kumwangalia mwanamke kama wenzo tu inaelekea kushindwa na kukataliwa.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyasema hayo katika kikao na maafisa wa ngazi za juu walioshiriki Kongamano la Kimataifa la Wanawake Wenye Taathira na Ushawishi; na sambamba na kueleza alivyofurahishwa kuona Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa mwenyeji wa kongamano la wanawake wenye ushawishi kutoka nchi mbalimbali amesema: Ninatumai kwamba wanawake waliohudhuria mkutano huu wataweza kutafakari kwa pamoja, kushirikiana na kuwa na mtazamo mmoja ili kuweza kupiga hatua kwa ajili ya kupatikana haki stahiki za wanawake duniani.
Seyyid Ebrahim Raisi aidha ameeleza matumaini yake kuwa wanawake waliohudhuria kongamano hilo la kimataifa wataweza kutumia tajiriba adhimu iliyopata Jamhuri ya Kiislamu ya Iran baada ya Mapinduzi ya Kiislamu katika uga wa haki za wanawake na kupewa umuhimu wanawake katika jamii na kuanzisha mashirikiano na mshikamano wenye manufaa.

Rais Raisi akihutubia kongamano la kimataifa la Wanawake wenye Ushawishi

Halikadhalika, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameeleza kuwa mkutano huo na mazungumzo yatakayofanywa yataweza kufungua njia za ushirikiano kati ya nchi na mataifa, na akabainisha kwa kusema: sisi hatuna shaka kwamba wanaume na wanawake wanatofautiana kwa msingi wa uumbwaji, lakini hakuna tofauti yoyote baina ya wanaume na wanawake kwa msingi wa ubinadamu.
Seyyed Ebrahim Raisi amesisitiza kuwa wanaume na wanawake hawana tofauti katika kufikia vilele vya utukufu wa kiutu na kwamba yeyote atakayefanya jitihada zaidi katika njia hiyo atafikia vilele vya utukufu wa maadili, umaanawi na ubinadamu.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Rais wa Iran amesema: "hatuoni tukio lolote muhimu la kihistoria ambalo wanawake hawakutoa mchango muhimu ndani yake" na akasisitiza kwa kusema,haipasi mwanamke kuwa mtu wa pembeni au kutengwa katika jamii.
Aidha ameongezea kwa kusema: Tafsiri sahihi kuhusu mwanamke ni kwamba mwanamke na mwanamme wote wawili ni wanadamu, na kuna hata wanawake ambao wana taathira kwa wanaume pia.../