Raisi: Jeshi la IRGC limesitisha shari za magaidi katika eneo
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria hatua ya Bunge la Ulaya dhidi ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kueleza kuwa jeshi la IRGC limekabiliana na magaidi na kuzima shari za magaidi katika eneo la Asia Magharibi.
Rais Sayyid Ebrahim Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema leo katika kikao cha Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge) cha kujadili mswada wa bajeti ya serikali yake kwa mwaka ujao wa 1402 kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani kwamba hakunan jeshi na vikosi vyovyote vya ulinzi ambavyo vimefanya juhudi kwa kiwango kilichofanywa na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) katika kukabiliana na ugaidi na kusitisha shari za magaidi katika eneo.
Raisi ameongeza kuwa, nchi za eneo na pia viongozi wa ngazi ya juu katika eneo lote hili wanafahamu suala hili kwama jeshi la IRGC limetoa mchango mkubwa na kuwa mstari wa mbele katika vita dhidi ya ugaidi. Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameeleza kuwa, hali ya mambo hivi sasa nchini Iran na Asia Magharibi ingekuwa nyingine kama asingekuwepo Haj Qassim Soleimani na wanajihadi wenzake. Rais Ebrahim Raisi amepongeza jitihada za jeshi la SEPAH na kueleza kuwa wale wanaotaka kulilaumu jeshi hili lenye nguvu juhudi zao hizo za kukata tamaa zitagonga mwamba kama yalivyofeli mahesabu ya karne.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aidha ameashiria hali ya mambo nchini hivi sasa na kueleza kuwa, kufikia ukuaji wa kiuchumi wa asilimia nne ni moja ya mafanikio ya serikali mwaka huu ambapo sera hiyo itaendelea pia mwaka ujao.
Rais Raisi ameongeza kuwa, ukuaji wa uwekezaji vitega uchumi na kupungua kwa mfumuko wa bei na kuongezeka uzalishaji ni miongoni mwa mafanikio mengine ya serikali katika mwaka huu wa 1401 na hivi sasa tunashuhudia ukuaji wa suhula na zana za uzalishaji wa asilimia 55."