Raisi: Kuivunjia heshima Qurani ni tusi kwa dini za mbinguni, utu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i93348-raisi_kuivunjia_heshima_qurani_ni_tusi_kwa_dini_za_mbinguni_utu
Rais wa Iran amesema vitendo vya karibuni vya kuvunjia heshima Qurani Tukufu katika nchi kadhaa za Ulaya ni tusi kwa dini zote za mbinguni zenye asili ya Nabii Ibrahim (AS), na kwa jamii yote ya wanadamu.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jan 27, 2023 02:48 UTC
  • Raisi: Kuivunjia heshima Qurani ni tusi kwa dini za mbinguni, utu

Rais wa Iran amesema vitendo vya karibuni vya kuvunjia heshima Qurani Tukufu katika nchi kadhaa za Ulaya ni tusi kwa dini zote za mbinguni zenye asili ya Nabii Ibrahim (AS), na kwa jamii yote ya wanadamu.

Rais Ebrahim Raisi alisema hayo jana Alkhamisi akihutubia kongamano la kitaifa lililofanyika hapa Tehran na kuongeza kuwa, vitendo vya kiwendawazimu vya kuyavunjia heshima Matukufu ya Kiislamu vinafanyika kwa kisingizio cha uhuru wa maoni, katika nchi za Ulaya zinazojinadi kuwa watetezi wa haki za binadamu.

Rais Raisi amebainisha kuwa, "Vitendo hivi vya kihaini na matukio mengine yanayofanywa kwa sura hiyo ya uhuru wa kujieleza, yanahesabiwa kuwa aina mbaya zaidi ya tusi kwa ubinadamu."

Jumatatu iliyopita, Edwin Wagensveld, mwanasiasa wa mrengo wa kulia na mwenye chuki kubwa dhidi ya Uislamu wa Uholanzi, kwa kejeli dharau na majivuno alichana na kuchoma moto kurasa za Qurani Tukufu katika mji wa Hague.

Hii ni siku chache baada ya mwanasiasa mwengine mwenye misimamo ya kufurutu ada wa Denmark, Rasmus Paludan, kuchoma moto nakala ya Kitabu Kitakatifu cha Mwenyezi Mungu nje ya ubalozi wa Uturuki katika mji mkuu Sweden, Stockholm. 

Vitendo hivi vimelaaniwa vikali na Waislamu pamoja na nchi na taasisi za Kiislamu duniani kote, ambapo serikali za Sweden na Uholanzi zimekosolewa kwa kuunga mkono vitendo hivyo viovu.

Rais Ebrahi Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, hakuna mtu yoyote katika sehemu yoyote ile ya dunia anapaswa kutetea na kuunga mkono kitendo kiovu cha kukivunjia heshima Kitabu Kitakatifu.