Aliyeshambulia ubalozi wa Jamhuri ya Azerbaijan mjini Tehran akamatwa
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i93366-aliyeshambulia_ubalozi_wa_jamhuri_ya_azerbaijan_mjini_tehran_akamatwa
Polisi mjini Tehran wanasema wamemkamata mtu mmoja aliyempiga risasi mlinzi kuwajeruhi wengine wawili baada ya kuingia katika ubalozi wa Jamhuri ya Azerbaijan katika mji mkuu wa Iran siku ya Ijumaa asubuhi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 27, 2023 08:57 UTC
  • Aliyeshambulia ubalozi wa Jamhuri ya Azerbaijan mjini Tehran akamatwa

Polisi mjini Tehran wanasema wamemkamata mtu mmoja aliyempiga risasi mlinzi kuwajeruhi wengine wawili baada ya kuingia katika ubalozi wa Jamhuri ya Azerbaijan katika mji mkuu wa Iran siku ya Ijumaa asubuhi.

Mkuu wa polisi mjini Tehran Brigedia Jenerali Hossein Rahimi alisema, "Mtu huyo aliingia katika ubalozi wa Jamhuri ya Azerbaijan leo asubuhi na kuanza kufyatua risasi na kisha kumuua mtu mmoja na kuwajeruhi wengine wawili."

Amesema polisi walichukua hatua za haraka na kumkamata mshambuliaji huyo na kuongeza kuwa uchunguzi unaendelea.

Kwa mujibu wa mkuu wa polisi wa Tehran, mshambuliaji huyo aliingia katika ubalozi huo akiwa na watoto wawili wadogo.

Jenerali Rahimi alisema "katika uchunguzi wa awali, mshambuliaji alisema kuwa motisha yake ilikuwa matatizo ya kibinafsi na ya kifamilia," na ameongeza kuwa mwanamume huyo ni Muirani aliyemuoa mwanamke wa Jamhuri ya Azerbaijan.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Nasser Kan'ani

Jenerali Rahimi aliongeza kuwa mwanaume huyo anadai mke wake ameshikiliwa katika ubalozi huo kwa muda wa miezi tisa.

Wizara ya mambo ya Nje ya Jamhuri ya Azerbaijan imetoa taarifa, ikisema kwamba mkuu wa huduma ya usalama ya ubalozi huo aliuawa kwa kupigwa risasi katika tukio hilo.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Nasser Kan'ani amelaani vikali shambulio hilo na kutoa pole kwa familia ya wahanga na serikali ya Jamhuri ya Azerbaijan na watu wake.

Aidha amesema kwa amri ya maafisa wa kisiasa na usalama, suala hilo linafuatiliwa kwa kipaumbele cha juu ili motisha ya mshambuliaji iwe wazi.

Akibainisha kuwa uchunguzi wa awali unaonyesha motisha za kibinafsi ndizo zilizohusika na shambulio hilo, Kan'ani alivitaka vyombo vya habari kujiepusha na uvumi.