Jan 29, 2023 02:37 UTC
  • Kadkhodaei: Operesheni ya kumsaka Pompeo na Trump itaendelea hadi haki ipatikane

Mjumbe wa Baraza la Walinzi wa Katiba nchini Iran ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kwamba mchakato wa kuwafuatilia rais na waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Marekani unaendelea kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya maafisa wa Iran na Iraq.

Mike Pompeo, waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Marekani, amekiri katika kumbukumbu zake kwamba alihusika katika kitendo cha kigaidi na kihalifu cha jeshi la Marekani cha mauaji ya Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran.

Luteni Jenerali Qassem Soleimani, kamanda wa zamani wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, ambaye tarehe 3 Januari, 2020 alikuwa safarini nchini Iraq kwa mwaliko rasmi wa serikali ya nchi hiyo, pamoja na Abu Mahdi Al-Muhandis, aliyekuwa naibu mkuu wa jumuiya maarufu ya uhamasishaji ya Al-Hashd al-Shaabi ya Iraq na wenzao 8 waliuawa shahidi katika shambulio la anga la jeshi vamizi la Marekani karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad, Iraqi.

Abbas Ali Kadkhodaei, mjumbe wa Baraza la Walinzi wa Katiba, ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kwamba: "Mchakato wa kuwasaka na kuwafuatilia Donald Trump na Mike Pompeo, rais na waziri zamani wa mambo ya nje wa Marekani, unaendelea kwa uhalifu wa kufanya mauaji dhidi ya maafisa rasmi Iran na Iraq." 

Trump na Pompeo

Kadkhodaei ambaye ni mkuu wa kamati maalumu ya kisheria na kimataifa ya kufuatili mauaji ya kigaidi ya Jenerali Haj Qassem Soleimani, ameandika kwamba: "Msako wa Pompeo na Trump unaendelea hadi haki itakapotendeka."

Mauaji ya Luteni Jenerali Qassim Soleimani, kama ilivyokiri Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon), yalifanyika kwa amri ya  Rais Donald Trump wa Marekani ni mfano wa wazi kabisa wa jinai za kivita za serikali ya kigaidi ya Marekani na kilele cha chuki na uadui dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.