Kan'ani: Hatima ya utawala bandia wa Israel ni kusambaratika
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameashiria matukio ya hivi karibuni katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na kusisitiza kuwa, kusambaratika kuko katika dhati na asili ya utawala bandia wa Israel.
Umepita mwezi sasa tangu kuanza kazi kwa baraza jipya la mawaziri la serikali ya Benjamin Netanyahu katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu (Israel); ambapo katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita kumeshuhudiwa mivutano zaidi ya ndani na mapigano yakijiri kati ya Wazayuni na Wapalestina.
Katika upande wa ndani, wazayuni wamekuwa wakiandamana mara kwa mara dhidi ya Netanyahu na baraza lake la mawaziri huku makumi ya maelfu ya watu wakiandamana katika miji mbalimbali nyakazi za usiku.
Katika uga wa nje pia, ghasia vitendo vya uchupaji mipaka vya Wazayuni dhidi ya Wapalestina vimewafanya wanamuqawama kutekeleza oparesheni nyingi za kiwango cha juu ndani ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu ambapo tarehe 27 mwezi Januari mwaka huu wanamapambano wa Palestina waliwaangamiza Wazayuni 11 na kuwajeruhi wengine karibu 20.
Shirika la habari la IRNA limeripoti kuwa, Nasser Kan'ani Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kuwa: Hatua za uharibifu za utawala wa Kizayuni dhidi ya mhimili wa muqawama hazitauzuia utawala huo na kusambaratika.
Kan'ani ameongeza kuwa, kwa utawala unaokumbwa na migogoro mikubwa ya ndani na kwa unaokabiliwa na mapambano ya wapigania uhuru na ukombozi wa Palestina katika maeneo 3 ya Gaza, Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na ardhi 1948, kujihusisha na vitendo vya maudhi dhidi ya Mhimili wa Muqawama hakutauokoa utawala huo haramu.