Iran: Ni haki yetu kujibu vikali vitisho na vitendo viovu vya Israel
Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel ndio wa kubeba dhima ya shambulio la kkigaidi la ndege isiyo na rubani (drone) lililolenga karakana ya zana za kijeshi mjini Isfahan Iran na kusisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ina haki ya kujibu vikali vitisho vyovyote na kile kitendo kisicho cha haki cha utawala wa Tel Aviv.
Amir Saied Iravani amesema hayo katika barua yake ya Jumatano kwa Rais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Katibu Mkuu wa umoja huo, zikiwa ni siku chache baada ya mfumo wa ulinzi wa anga wa Iran kufanikiwa kukamata kwa ufanisi wa hali ya juu na kutungua droni mbili kati ya tatu za kijeshi zilizotumiwa na utawala ghasibu wa Israel kufanya uchokozi dhidi ya Iran.
Amesema uchunguzi wa awali unaonesha kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel ndio uliohusika na jaribio la kivamizi huko Isfahan.
Balozi Iravani amesema: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inahifadhi haki yake halali na ya kimsingi, inayokubaliwa na sheria za kimataifa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa, ya kujihami na kulinda usalama wa taifa lake na kujibu vikali vitisho au vitendo viovu vya aina yoyote ile vinavyofanywa na utawala wa Israel, popote na wakati wowote itakapoona panafaa."

Aidha amesisitiza pia kuwa, vitisho vya Israel vya kutumia nguvu dhidi ya miundombinu muhimu ya Iran vikiwemo vituo vyake vya amani vya nyuklia ni ukiukaji wa sheria za kimataifa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa. Amesema, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni, Benjamin Netanyahu amekiri kuhusika Tel Aviv katika vitendo vya kihalifu, hujuma na ugaidi nchini Iran.
Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa, shambulio la Isfahan si tukio la kwanza bali utawala wa Israel umekuwa ukitoa vitisho vya mara kwa mara vya kutumia mabavu, kutenda jinai na kuendesha vitendo vya kigaidi ndani ya ardhi ya Iran.
Amesema, lazima Israel iwajibike kwa vitendo vyote vya jinai na kigaidi vinavyofanywa dhidi ya Iran na ibebe dhima ya matokeo yoyote ya ugaidi wake huo.