Iran yalaani ukandamizaji wanaofanyiwa wanawake katika nchi za Magharibi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i93630-iran_yalaani_ukandamizaji_wanaofanyiwa_wanawake_katika_nchi_za_magharibi
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje tya Iran amelaani hatua kandamizi ya Baraza la Congress la Marekani ya kumtoa Mbunge Ilhan Omar katika Kamati ya Mambo ya Nje ya baraza hilo na kusema kuwa, huo ni unyanyasaji wa kitaasisi uliofanywa na Bunge la Marekani kwa ajili ya kukandamiza sauti za wanawake.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Feb 03, 2023 09:56 UTC
  • Iran yalaani ukandamizaji wanaofanyiwa wanawake katika nchi za Magharibi

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje tya Iran amelaani hatua kandamizi ya Baraza la Congress la Marekani ya kumtoa Mbunge Ilhan Omar katika Kamati ya Mambo ya Nje ya baraza hilo na kusema kuwa, huo ni unyanyasaji wa kitaasisi uliofanywa na Bunge la Marekani kwa ajili ya kukandamiza sauti za wanawake.

Ilhan Omar, mbunge mwanamke, Muislamu anayevaa Hijab ambaye ameingia bungeni huko Marekani kwa tiketi ya chama cha Democratic ametolewa katika Kamati ya Mambo ya Nje ya Baraza la Congress kutokana na kutumia haki yake ya kulalamikia ukatili wa utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina. 

Katika upigaji kura uliolalamikiwa sana, Baraza la Wawakilishi la Marekani limemtoa Ilhan Omar kwenye kamati hiyo kwa kura 218 za ndio dhidi ya kura 211 za hapana. Bunge hilo hivi sasa linadhibitiwa na chama cha Donald Trump, cha Republican.

Nasser Kan'ani Chafi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran

 

Mwaka 2019, Ilhan Omar alitumia mtandao wa Twitter, kuwalaumu waungaji mkono wa utawala wa Kizayuni wa Israel akisema: "Kila wanachofanya kinalenga kumsaidia kipenzi chao, Benjamin."

Shirika la habari la Iran Press limemnukuu Nasser Kan'ani Chafi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran akisema leo Ijumaa kwamba, kutolewa Ilhan Omar katika Kamati ya Mambo ya Nje ya Congress ya Marekani ni unyanyasaji wa kibunge huko Marekani kwa ajili ya kukandamiza sauti ya mbunge mwanamke anayetumia haki yake kueleza anachoona ni sawa.

Ilhan Omar ni mkimbizi kutoka Somalia. Ni katika wanawake wa kwanza Waislamu wanaovaa vazi la staha la Hijab, kuwahi kuingia Bungeni nchini Marekani. Mara nyingi amekuwa akitishiwa kuuawa na anakumbwa na maneno ya kejeli na vitisho mbalimbali kutoka kwa magenge ya Wazungu wenye misimamo mikali huko Marekani.