Amir-Abdollahian: Sera ya vikwazo ya Marekani itashindwa tu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i93682-amir_abdollahian_sera_ya_vikwazo_ya_marekani_itashindwa_tu
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian, amesema sera ya Marekani ya vikwazo vya upande mmoja na vya uonevu itashindwa tu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 05, 2023 00:03 UTC
  • Amir-Abdollahian: Sera ya vikwazo ya Marekani itashindwa tu

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian, amesema sera ya Marekani ya vikwazo vya upande mmoja na vya uonevu itashindwa tu.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, Hossein Amir- Abdollahian, ameyasema hayo katika mkutano na Waziri wa Mambo ya Nje wa Cuba Bruno Rodríguez waliofanya mjini Havana na akasisitiza kwamba: matukio ya Julai, 2022 yameonyesha kuwa silaha ya vikwazo haina athari na Marekani ilichochea uasi kwa ajili ya kufanikisha malengo yake maovu.
Katika mkutano huo, Amir Abdullahian ametilia mkazo pia umuhimu wa uhusiano kati ya nchi mbili.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Cuba amesema, amefurahishwa na kuwepo kwa ujumbe wa Iran mjini Havana na akaongeza kuwa, safari ya ujumbe huo ni fursa ya kuthamini na kuenzi uungaji mkono wa Iran kwa Cuba katika kukabiliana na mzingiro wa pande zote wa kiuchumi dhidi ya nchi hiyo.
Waziri Amir-Abdollahian alipowasili Havana

Aidha, Rodrigues amelaani vikwazo vya upande mmoja dhidi ya Iran na uingiliaji wa masuala ya taifa hili.

Vilevile ameongeza kuwa, Cuba inaunga mkono haki ya nchi zote kunufaika na nishati ya nyuklia kwa malengo ya amani.
Katika mkutano wao huo, mawaziri wa mambo ya nje wa Iran na Cuba wamezungumzia pia masuala ya pande mbili na ya kimataifa.
Kabla ya mazungumzo yake na Rodrigues, Amir-Abdollahian alikutana na kuzungumza na Rais wa Cuba Miguel Diaz-Canel.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran aliwasili Havana, mji mkuu wa Cuba, Jumamosi jioni na kukaribishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Masuala ya Kimataifa wa Wizara ya Mambo ya Nje ya ya nchi hiyo.
Mkuu wa vyombo vya diplomasia vya Iran na ujumbe alioandamana nao hapo awali walitembelea Nicaragua na Venezuela na kufanya mashauriano na maafisa wa nchi hizo kuhusu njia za kupanua uhusiano hususan ushirikiano wa kiuchumi.
Kabla ya hapo, Amir-Abdollahian alikuwa na safari fupi nchini Mauritania ambako alikutana na kuzungumza na rais na waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo ya kaskazini magharibi mwa Afrika.../