Msamaha wa Kiongozi Muadhamu kwa wafungwa wa machafuko ya hivi karibuni
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i93752-msamaha_wa_kiongozi_muadhamu_kwa_wafungwa_wa_machafuko_ya_hivi_karibuni
Kwa mnasaba wa kuwadia maadhimisho ya miaka 44 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na sikukuu za mwezi wa Rajab, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa msamaha na punguzo la vifungo kwa makumi ya maelfu ya watuhumiwa na wafungwa wa machafuko ya hivi karibuni hapa nchini.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 06, 2023 22:51 UTC
  • Msamaha wa Kiongozi Muadhamu kwa wafungwa wa machafuko ya hivi karibuni

Kwa mnasaba wa kuwadia maadhimisho ya miaka 44 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na sikukuu za mwezi wa Rajab, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa msamaha na punguzo la vifungo kwa makumi ya maelfu ya watuhumiwa na wafungwa wa machafuko ya hivi karibuni hapa nchini.

Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameidhinisha pendekezo la Mkuu wa Idara ya Mahakama ya Iran, Gholam Hossein Mohseni Ejei la kupunguziwa vifungo au kuachiwa huru makumi ya maelfu ya wafungwa wa Kiirani waliokuwa wakitumikia vifungo katika magereza mbalimbali hapa nchini.

Sehemu moja ya barua ya Hujjatul-Islam Walmuslimin Gholam Hossein Mohseni Ejei, Mkuu wa Idara ya Mahakama ya Iran kwa Kiongozi Muadhamu, imeeleza kuwa: Katika matukio ya hivi karibuni baadhi ya wananchi hususan vijana walifanya vitendo visivyo sahihi kutokana na kuathirika na propaganda za maadui na hivi sasa wengi wao wamejuta kwa vitendo hivyo na wanaomba msamaha, hasa baada ya kufahamika njama za maadui wa kigeni na makundi yaliyo dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu.

Gholam Hossein Mohseni Ejei

Sura ya 110 ya Katiba ya Iran inampa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu mamlaka ya kupunguza au kuwasamehe wafungwa kutokana na pendekezo la Mkuu wa Idara ya Mahakama ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Tangu mwanzo wa kipindi chake cha uongozi mwaka 1368 Hijria Shamsia, kwa nyakati tofauti, Ayatullah Ali Khamenei amewasamehe baadhi ya wafungwa na kuwapunguzia adhabu wengine. Hata hivyo, mwafaka wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu wa kusamehewa na kuwapunguzia adhabu wengi kati ya watuhumiwa na waliopatikana na hatia ya kuhusika na machafuko ya hivi karibuni una nukta muhimu zinazopaswa kuangaziwa zaidi na ni kielelezo cha tadbiri, busara na kuona mbali kwa ajili ya kuimarisha Mapinduzi na Iran ya Kiislamu. Maadui wa Iran ya Kiislamu walitumia uwezo wao wote kuushambulia Mfumo na wananchi katika machafuko ya hivi karibuni, lakini kama ilivyokuwa miaka ya nyuma, njama hiyo pia ilifeli, na kwa mara nyingine tena umoja wa wananchi na nguvu ya Jamhuri ya Kiislamu vimewazuia kufikia malengo yao.

Nukta nyingine muhimu kuhusu hatua ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya kusamehe na kupunguza adhabu za watuhumiwa na wale waliopatikana na hatia ni kwamba msamaha huu ni fursa kwa baadhi ya watu waliohadaiwa na njama na vita vya kisaikolojia vya maadui na kujihusisha na uhalifu na vitendo viovu kwa kuathiriwa na vita mseto vya mahasimu wa Iran ya Kiislamu. Kwa hivyo, msamaha wa Kiongozi Muadhamuu unaweza kutathminiwa kuwa ni matokeo ya huruma ya Kiislamu na hatua yenye taathira kubwa kwa ajili ya kudumisha umoja katika jamii, kwa sababu msingi wa Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ni rehma na msamaha kwa baadhi ya watu wanaoteleza katika jamii.

Nukta nyingine muhimu ya kuashiriwa ni ulazima wa kulindwa umoja na mshikamano wa kitaifa. Katika matukio na misukosuko ya hivi karibuni hapa nchini, maadui walijaribu kuzusha hitilafu baina ya matabaka na kaumu mbalimbali nchini Iran, jambo ambalo lilishindwa kama ilivyokuwa huko nyuma, kutokana na stratijia na tadbiri ya Kiongozi Muadhamu, umakini wa vyombo vya upelelezi na usalama, na umoja wa wananchi.

Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Nukta nyingine muhimu ni kwamba msamaha na kupunguzwa kwa adhabu kwa waliopatikana na hatia ya kuhusika na ghasia za hivi karibuni, kwa mara nyingine tena kunaonyesha uthabiti na usalama uliopo katika Mfumo wa Kiislamu wa Iran. Kwa hakika tunaweza kusema kuwa, hatua hii inaashiria kwamba Mfumo wa Kiislamu wa Iran sio tu kwamba haujadhoofishwa, bali umewasamehe watu hao waliopatikana na hatia ambao wamejuta na kuomba msamaha kwa mienendo yao mibaya, ukiwa katika nafasi nzuri, madhubuti na yenye nguvu kubwa.