Brigedia Jenerali Sharif: Wahusika wa shambulio lililoshindwa dhidi ya Isfahan watajuta
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i93776-brigedia_jenerali_sharif_wahusika_wa_shambulio_lililoshindwa_dhidi_ya_isfahan_watajuta
Msemaji wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (Sepah) amesema kuwa, wahusika wa shambulio lililofeli hivi karibuni kwenye moja ya karakana za Wizara ya Ulinzi ya Iran katika mji wa Isfahan katikati mwa Iran, bila shaka watajutia kitendo hicho.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 07, 2023 06:58 UTC
  • Brigedia Jenerali Ramazan Sharif
    Brigedia Jenerali Ramazan Sharif

Msemaji wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (Sepah) amesema kuwa, wahusika wa shambulio lililofeli hivi karibuni kwenye moja ya karakana za Wizara ya Ulinzi ya Iran katika mji wa Isfahan katikati mwa Iran, bila shaka watajutia kitendo hicho.

Brigedia Jenerali Ramazan Sharif, msemaji wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran amesema katika mahojiano yake na televisheni ya al-Masirah kwamba, adui anajua matokeo ya vitendo vyake na anafahamu kwamba hatua yoyote dhidi ya Iran itakabiliwa na jibu kali.

Tarehe 28 Januari quadcopter tatu ndogo ziliruka kwa nia ya kufanya shambulio kwenye moja ya karakana za Wizara ya Ulinzi ya Irani katika mkoa wa Isfahan, lakini shambulio hilo  lilifeli na halikusababisha maafa ya binadamu, lakini liliharibu paa la kiwanda hicho kwa kiasi kidogo. 

Uchunguzi wa kiufundi wa mabaki ya mmoja wa ndege hizo ndogo zisizo na rubani zilizodunguliwa na jeshi la Iran umetoa taarifa muhimu kwa taasisi za usalama za Jamhuri ya Kiislamu.

Kupitia uchambuzi wa vipengele vya mabaki ya ndege hizo umebaini kwa usahihi mahali zilikotengenezwa na kudhihirisha masuala mengine muhimu kuhusu waliohusika na hujuma hiyo.

Taarifa iliyotolewa awali na Wizara ya Ulinzi ya Iran ilieleza kuwa, moja ya droni hizo ilishushwa chini na mfumo wa ulinzi wa anga wa Iran katika shambulio hilo huku nyingine mbili zikitunguliwa.