Iran yazindua satalaiti mbili mpya ambazo imejiundia yenyewe
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imezindua satelaiti mbili ambazo imejiundia yenyewe moja ikiwa ni ya mawasiliano na nyingine ya kupiga picha.
Satalaiti hizo mbili ambazo zimeundwa kwa tekenolojia ya hali ya juu zinajulikana kama Nahid-2 na Tolou-3 na zilionyeshwa katika hafla ya Jumanne katika mji mkuu Tehran kwa mnasaba wa Siku ya Kitaifa ya Anga za Juu ya Iran.
Satelaiti ya mawasiliano ya Nahid-2 imetengenezwa na Kituo cha Utafiti wa Anga za Juu cha Iran kwa ombi la Wakala wa Anga za Juu wa Iran (ISA).
Satalaiti hiyo inaweza kudumu katika anga za juu kwa muda wa miaka 2, na itakuwa ikizunguka kwa urefu wa kilomita 500 juu ya uso wa dunia
Nahid-2 itatekeleza majukumu kadhaa ya mawasiliano kama vile mawasiliano ya simu kwa wakati mmoja na pia itaweza kuhifadhi na kulinda data muhimu. Satelaiti hiyo tayari imefaulu majaribio yake yote na iko tayari kurushwa katika anga za mbali
Satelaiti ya Tolou-3 nayo ni satelaiti ya kupiga picha iliyozinduliwa na Wakala wa Anga za Juu wa Iran (ISA) na imeundwa na Shirika la Iran la Viwanda vya Kielektroniki.
Ikiwa na uzito wa kilo 150, Tolou-3 inaaminika kuwa satelaiti nzito zaidi kuwahi kutengenezwa nchini Iran.
Tolou-3 ina uwezo wa kunasa picha nyeusi na nyeupe na pia picha za rangi zenye ubora wa hali ya juu.
Satelaiti hiyo ambayo inategemea sana vifaa na zana zinazozalishwa na makampuni ya Kiirani inatarajiwa kurushwa katika anga za juu hivi karibuni.
Iran ilirusha satelaiti yake ya kwanza ya Omid mnamo 2009 na satelaiti yake ya Rasad ilitumwa kwenye obiti mnamo 2011.
Mnamo mwaka wa 2012, Jamhuri ya Kiislamu ilifanikiwa kurusha katika anga za mbali satelaiti yake ya tatu iliyotengenezwa nchini.
Mnamo Aprili 2020, Iran ilitangaza kurusha kwa mafanikio satelaiti yake ya kwanza ya kijeshi na mnamo Machi 2022, ikavurumisha satelaiti yake ya pili ya kijeshi angani.
Mafanikio hayo yote yamepatikana pamoja na kuwa nchi hii imewekewa vikwazo na madola ya Magharibi yakiongozwa na Marekani.