Uhusiano wa kiuchumi wa Iran na China katika mkondo mpya
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i94054-uhusiano_wa_kiuchumi_wa_iran_na_china_katika_mkondo_mpya
Sambamba na safari ya Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini China, kumefanyika kikao cha pamoja cha wafanyabiashara wa wa pande mbili katika jiji la Beijing.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 14, 2023 09:21 UTC
  • Uhusiano wa kiuchumi wa Iran na China katika mkondo mpya

Sambamba na safari ya Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini China, kumefanyika kikao cha pamoja cha wafanyabiashara wa wa pande mbili katika jiji la Beijing.

Mehdi Safari, Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran anayesimamia Diplomasia ya Uchumi amesema katika kikao cha pamoja cha wafanyabiashara kwamba, safari ya Rais wa Iran nchini China inaweza kusukuma mbele kwa haraka gurudumu la utekelezwaji wa mipango na ushirikiano wa kibiashara na kiuchumi baina ya nchi mbili hizi.

Rais Sayyid Ebrahim Raisi wa Iran aliwasili China alfajiri ya leo na kupokewa katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Beijing na Waziri wa Utamaduni na Utalii wa nchi hiyo. Hii ni ziara rasmi ya kwanza ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini China baada ya kupita miaka 20. Rais wa Iran yupo nchini China akiitikia mwaliko wa Rais wa nchi hiyo Xi Jinping ambapo moja ya malengo ya safari hiyo ni kufuatilia utekelezwaji wa hati ya mkakati ya miaka 25 wa ushirikiano baina ya nchi mbili hizi.

Marais wa Iran na China sambamba na kukutana na kufanya mazungumzo mjini Beijing wametiliana saini hati 20 za ushirikiano katika nyanja mbalimbali. Hati hizo zinajumuisha ushirikiano baina ya Iran na China katika nyuga mbalimbali kama kilimo, utalii, mawasiliano, teknolojia, mazingira, biashara ya kimataifa, afya, usafirishaji bidhaa nje ya nchi, tiba, vyombo vya habari, michezo na kadhalika.

 

China ikiwa taifa kubwa la bidhaa za uchumi duniani, katika miaka iliyopita, imekuwa na ushirikiano mkubwa wa kibiashara na Iran tena hata katika kipindi cha kufikia kilele vikwazo vya kidhalimu vya madola ya Magharibi dhidi ya Tehran. Katika miaka yote hii China imebakia kuwa mshirika mzuri wa kibiashara wa Iran. Hata hivyo pamoja na hayo yote, Iran na China kwa kuzingatiwa uwezo mkubwa zilionazo zinaweza kustawisha zaidi uhusiano na ushirikiano baina yao hasa katika uga wa kibiashara.

China imetuma Iran tani milioni 29.2 za bidhaa zenye thamani ya dola bilioni 25.3 katika kipindi cha miezi kumi iliyopita na kuwa taifa lenye kiwango kikubwa zaidi cha mabadilishano ya kibiashara na Iran. Aidha China imekuwa mnunuzi mkubwa zaidi wa bidhaa za Iran baada ya kununua bidhaa zenye thamani ya dola bilioni 12 na milioni 806 za Iran. Kiwango hicho kinaelezwa kuwa ni ongezeko la asilimia 10 ikilinganishwa na kipindi hiki mwaka uliopita.

Wakati huo huo uingizaji wa bidhaa za China nchini Iran umeongezeka kwa asilimia 33 jambo ambalo linathibitisha juu ya kuweko ushirikiano imara wa kibiashara baina ya mataifa haya mawili.

Sera za Iran katika uga wa kuwa na mtazamo wa pande kadhaa, uzingatiaji wa Iran kwa eneo la mashariki, uanachama wake katika Jumuiya ya Shanghai, ushirikiano wa kimataifa wa Iran na mataifa ya Asia, mahusiano wa kihistoria ya Tehran na Beijing ni miongoni mwa masuala ambayo yamepelekea kuongezeka ushirikiano wa kibiashara na kiuchumi baina ya mataifa haya mawili.

 

Hata hivyo kwa kuzingatia ukubwa wa kiuchumi wa China na uhusiano mzuri wa Iran na taifa hilo, inatarajiwa kiwango cha uwezekezanio wa China hapa nchini kiongezeke. Katika kipindi cha takribani mwaka uliopita, China imefanya uwekezaji wa moja kwa moja nchini Iran wenye thamani ya dola bilioni 200 na kwa muktadha huo kushika nafasi ya nne baada ya Russia, Imarati na Uturuki.

Ni jambo lisilo na shaka kwamba, kuwa Iran katika nafasi nzuri kijiografia ni jambo linaloifanya izingatiwe kieneo na kimataifa hasa kutokana na kuhesabiwa kuwa daraja na kivuko baina ya bara la Asia, Ulaya na Afrika. Iran pia ni taifa lenye  kumiliki akiba na utajiri mkubwa wa mafuta na gesi na hivyo inaweza kuwa na nafasi muhimu katika kudhamini nishati na usalama wake kwa ajili ya China.

Ni kwa kuzingatia ukweli huo, ndio maana safari ya Rais Ebrahim Raisi nchini China inahesabiwa na wajuzi wa mambo kuwa ina umuhimu wa aina yake na itaandaa mazingira mwafaka ya kuimarishwa zaidi uhusiano na ushirikiano baina ya mataifa haya mawili rafiki.