Iran inajiandaa kujibu mapigo ya kuwekewa vikwazo na Umoja wa Ulaya
(last modified Tue, 21 Feb 2023 03:39:54 GMT )
Feb 21, 2023 03:39 UTC
  • Iran inajiandaa kujibu mapigo ya kuwekewa vikwazo na Umoja wa Ulaya

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema ndani ya siku chache zijazo itatoa jibu la vikwazo vya hivi karibuni vilivyowekwa na Umoja wa Ulaya dhidi ya shakhsia 32 na taasisi mbili za Jamhuri ya Kiislamu.

Nasser Kan'ani, Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema karibu hivi, Iran itachapisha orodha mpya ya shakhsia na taasisi za Ulaya ambazo zitawekewa vikwazo na serikali ya Tehran, ikiwa ni katika kukabiliana na vikwazo vya hivi karibuni vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Kwa mujibu wa taarifa EU, shakhsia wa Iran waliowekwa kwenye kifurushi hicho kipya cha vikwazo kwa kisingizio cha kutoheshimiwa haki za binadamu ni pamoja na Waziri wa Utamaduni na Miongozo ya Kiislamu, Mehdi Esmaeili, Waziri wa Elimu, Yousef Nouri, na Naibu Kamanda na Msemaji wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC).

Aidha Umoja wa Ulaya umewaweka kwenye orodha yake hiyo mpya ya vikwazo baadhi ya Wabunge, baadhi ya wakuu wa idara za polisi na mahakama katika pembe mbalimbali za Iran, na vilevile maaskari gereza.

Mwishoni mwa mwezi uliopita wa Januari, Iran ilichukua hatua nyingine kama hiyo ya kujibu mapigo. Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ilichapisha orodha iliyojumuisha majina ya taasisi na makampuni 3, maafisa 22 wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya, pamoja na taasisi moja na maafisa 8 wanaohudumu au waliowahi kuhudumu katika serikali ya Uingereza. 

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ilieleza kuwa, watu na taasisi zilizojumuishwa katika orodha hiyo ni kutokana na kuhusika kwao kwa njia moja au nyingine katika kuunga mkono ugaidi na makundi ya kigaidi, kuchochea na kuhimiza vitendo vya kigaidi na ukatili dhidi ya wananchi wa Iran, kuingilia masuala ya ndani ya Iran, kueneza ghasia na machafuko nchini Iran, kuchapisha na kutangaza habari za uwongo dhidi ya Iran, na pia kushiriki katika njama za kuongeza vikwazo vya kidhalimu dhidi ya Wairani, jambo ambalo linachukuliwa kuwa ni ugaidi wa kiuchumi dhidi ya taifa la Iran.

Tags