Iran: Kusambaratika Israel hakuepukiki licha ya uungaji mkono wa US
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema utawala haramu wa Israel upo katika ncha ya kusambaratika na kutokomea, licha ya uungaji mkono.
Nasser Kan'ani alisema hayo jana Alkhamisi katika ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter na kufafanua kuwa, hatima ya utawala bandia wa Israel ni kusambaratika, pamoja na kuwa unakingiwa kifua na Marekani.
Amesema licha ya misaada na uungaji mkono wa Marekani, muitifaki mkubwa wa kistratejia wa Tel Aviv katika eneo la Asia Magharibi, lakini hakuna chembe ya shaka kuwa utawala huo pandikizi utaangamia.
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezionya nchi ambazo zinaanzisha uhusiano wa kawaida na Israel na kubainisha kuwa, Israel haina hadhi ya kuyafanya madola hayo yafanye uwekezaji na utawala huo za Kizayuni.
Kan'ani ameeleza bayana kuwa, kujikurubisha kwa Israel si tu kutayafanya madola yaliyoanzisha uhusiano wa kawaida na utawala huo wa kibaguzi kupata hasara kwenye mitaji yao, lakini pia thamani zao za kimaadili zitasambaratika.
Kauli ya Kan'ani imekuja siku moja baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa Israel, Yair Lapid kuonya kuwa, utawala huo wa Kizayuni umesalia na miezi michache usambaratike.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameongeza kuwa, hatua za uharibifu za utawala wa Kizayuni dhidi ya mhimili wa muqawama hazitauzuia utawala huo kusambaratika.