Kura ya maoni; Misingi yake na jinsi inavyotumiwa vibaya
Moja ya mada ambazo kwa kawaida huibuliwa na baadhi ya watu ndani ya nchi na vyombo vya habari vinavyoipinga Jamhuri ya Kiislamu nje ya nchi, wakati kunapoibuka matatizo katika nyanja za kisiasa na kiuchumi Iran, ni suala la kufanyika kura ya maoni.
Ombi la kufanyika kwa kura ya maoni hutolewa kwa misukumo tofauti. Kwa mfano, baadhi ya watu na makundi ndani ya nchi, wanaojiita wanamageuzi, walitaka kufanyika kura ya maoni ili kupunguza mamlaka ya baadhi ya taasisi rasmi za nchi kwa lengo la kujiongezea madaraka. Vombo vya habari vya maadui na wapizani pia vinatumia suala la kura ya maoni kama njia ya kuifutilia mbali Jamhuri ya Kiislamu ambayo ndio msingi wa kisiasa nchini Iran.
Katika miezi ya hivi karibuni, baada ya machafuko katika baadhi ya miji ya Iran, ambayo yaliendelea kwa kuungwa mkono na kuchochewa na madola ya Magharibi, suala la kufanyika kura ya maoni lilisikika tena na kupigiwa debe bila ya kuzingatia kanuni na namna inavyoweza kufanyika.
Awali ya yote, ikumbukwe kwamba kutokana na umuhimu wake, ukubwa na kuchukua kwake muda mrefu, ufanyikaji wa kura ya maoni unakusudiwa tu kwa masuala ya msingi na muhimu ya nchi; hivyo vyombo vya sheria na utendaji vya nchi haviwezi kuchelewesha maamuzi yao ili kusubiri kura ya maoni.
Pia, kura ya maoni katika sheria za msingi za mifumo yote ya kisiasa imeundwa kwa kutilia maanani suala la kulinda asili ya mfumo na utawala huo, na hakuna mfumo wa utawala, hata uwe wa kidemokrasia kiasi gani, unaoweka uhai na uwepo wake kwenye meza ili upigiwe kura ya maoni. Kwa mfano, karibu miaka 250 imepita tangu baada ya uhuru wa Marekani, lakini hakujawahi kufanyika kura ya maoni kuhusu mfumo wa kisiasa wa nchi hiyo. Nchi nyingine za Magharibi zinazodai kutetea demokrasia pia zina hali kama hiyo, yaani, hazijawahi kuwataka wananchi wapige kura ya maoni kuhusu mfumo wa kisiasa unaotawala. Nchi kama Uingereza kimsingi haina katiba iliyoandikwa na hakuna uwezekano wa kupiga kura ya maoni kuhusu suala la katiba nchini humo.

Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran Februari 1979 kumefanyika kura za maoni mara tatu hapa nchini kuhusiana na mfumo wa nchi na masuala muhimu ya kisiasa. Kura ya maoni ya kwanza nchini Iran baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ilifanyika tarehe 31 Machi 1979, na katika kura hiyo ya maoni, aina ya mfumo wa serikali ya Iran iliamuliwa kwa asilimia 98.2 ya kura za ndio na kuwa "Jamhuri ya Kiislamu".
Baada ya hapo, tarehe 3 Disemba 1979, Katiba ya kwanza ya Jamhuri ya Kiislamu iliidhinishwa na umma kupitia kura ya maoni. Katiba hiyo ilifanyiwa marekebisho baada ya miaka 10.
Marekebisho hayo nayo yaliwekwa mbele ya wananchi na kuidhinishwa katika kura ya maoni mnamo 28 Julai 1989.
Jambo lingine muhimu kuhusu kura ya maoni ni suala la masharti na namna inavyofanyika. Katika Katiba ya baadhi ya nchi kama vile Uswizi kuna uwezekano wa kukusanya saini kutoka kwa watu ili kuitisha kura ya maoni. Nchini Iran, hata hivyo, ombi la kura ya maoni linawezekana kwa kura ya angalau theluthi mbili ya wabunge. Kwa mujibu wa Kifungu cha 36 cha Sheria ya Kura ya Maoni katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kura ya maoni hufanyika kwa mapendekezo ya Rais au wajumbe mia moja wa Bunge au Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu na kuidhinishwa na angalau theluthi mbili ya idadi ya wawakilishi wote. Ibara ya 110 ya Katiba inataja amri ya kura ya maoni chini ya wajibu na mamlaka ya Kiongozi Muadhamu ambayo ina maana ya ulazima wa kupitishwa kwa azimio la Bunge na kutolewa kwa amri ya kura ya maoni na Kiongozi Muadhamu.
Kwa hivyo, katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, sheria na utaratibu wa kura ya maoni uko wazi, na historia ya kufanyika kura hiyo mara tatu inaonesha kuwa, tofauti na nchi za Magharibi zinazodai kutetea demokrasia, kura za maoni zimefanyika kuhusu masuala muhimu ya kisiasa nchini Iran.
Kuhusiana na hilo, Ayatullah Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika kikao chake na wanachuo siku ya Jumanne iliyopita alisema kumekuwepo na mtazamo usio wa uhalisia na madai yasiyo na msingi wa kielimu, na huku akiashiria kauli ya mmoja wa wanachuo hao alisema: “Tofauti na ilivyoelezwa kuwa ‘tunapaswa kupiga kura ya maoni kuhusu masuala mbalimbali tangu siku ya kwanza ili kusiwe tashwishi’, masuala mbalimbali ya nchi hayawezi kutajwa katika kura ya maoni, kwa sababu kila kura ya maoni inashughulisha nchi nzima kwa muda wa miezi sita. Pia, ni wapi ulimwenguni kura ya maoni inaweza kufanywa kwa ajili ya masuala yote?”