Tuhuma isiyo na msingi na jibu kali la Iran
Ali Shamkhani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa, ameashiria kwenye ukurasa wake binafsi katika mtandao wa Twitter, matamshi yaliyotolewa karibuni na Jake Sullivan, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani, kuwa iwapo Iran itajaribu kutengeneza bomu la nyuklia, Washington itatambua rasmi uamuzi wa Israel wa kukabiliana na hali hiyo.
Shamkhani amesema kukiri huko kunamaanisha kuwa Marekani itawajibika kubeba dhima ya vitendo vyote vya kigaidi vya utawala wa Kizayuni dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran na watu wake, na kwamba lazima ikubali matokeo yake. Ijumaa ya Mei 15, Jake Sullivan, Mshauri wa Usalama wa Taifa katika Ikulu ya White House, alitoa madai yasiyo na msingi kuhusu mpango wa amani wa nyuklia wa Iran na kusema Rais Joe Biden wa Marekani anasisitiza kuwa Iran haipaswi kupata "silaha za nyuklia". Aliendelea kuropoka na kudai kuwa Washington itaendelea kushirikiana na washirika wake na hasa utawala haramu wa Israel, katika kile alisema ni juhudi za kuizuia Iran kumiliki silaha za nyuklia.
Matamshi hayo ya kichochezi yanatolewa katika hali ambayo Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA, ambayo ni mamlaka pekee ya kisheria na yenye uwezo wa kusimamia shughuli za nyuklia, umesisitiza mara nyingi katika ripoti zake kwamba mpango wa nyuklia wa Iran unatekelezwa kwa malengo ya amani.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa ikisisitiza kuwa, kamwe haitasalimu amri mbele ya mashinikizo ya kidhalimu na kwamba itaendelea kutetea haki zake halali na za kisheria zikiwemo za nyuklia na kuwa itatoa jibu kali na la kipigo kwa chokochoko zozote za utawala ghasibu wa Israel na washirika wake.
Wachambuzi wengi wa mambo wanaamini kuwa, utawala wa Kizayuni hauna uwezo wa kuingia katika vita au kuchochea mivutano inayoweza kulipua hali ya mambo katika eneo kwa sababu hauna uwezo wa kustahamili matokeo yake.
Kupungua ushawishi na nguvu za utawala huo ni suala linalojadiliwa sana katika duru za Israel. Hali hiyo ya udhaifu wa Israel ilionekana wazi kufuatia vita vya Julai 2006 kati ya utawala huo ghasibu na Hizbullah nchini Lebanon na vile vile vita vya Upanga wa Quds vya mwezi Mei 2021. Hali imezidi kuwa ngumu kwa utawala huo tangu kuingia madarakani baraza la mawaziri la mrengo wa kulia linaloongozwa na Benjamin Netanyahu ambapo sasa viongozi na maafisa wa kijeshi wa utawala huo wanazungumza hadharani juu ya uwezekano wa kuangamia Israel katika siku zijazo.
Kwa mujibu wa gazeti la Yediot Aharonot, makombora ya majini ambayo Israel inakabiliana nayo katika vita vinavyokuja yana uwezo wa kulenga shabaha iliyo umbali wa kilomita 70-700 na tayari yamewekwa katika Ukanda wa Gaza, Lebanon, Syria, Yemen na Iraq.
Moja ya changamoto kubwa za utawala wa Kizayuni ni kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran licha ya mzingiro na vita vingi vilivyoanzishwa dhidi yake, imefanikiwa kufikia kiwango cha juu cha nguvu za kijeshi na maendeleo katika nyanja mbalimbali za teknolojia ya kijeshi na makombora, jambo ambalo limeimarisha mhimili wa muqawama na milingano ya kistratejia dhidi ya adui Mzayuni.
Kinyume na ilivyo Marekani na utawala wa Kizayuni, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haina malengo ya kijeshi katika mpango wake wa nyuklia, bali inazingatia matumizi ya nishati ya nyuklia katika maendeleo endelevu na wala haikubali kuwekewa vizingiti katika njia hiyo.
Sayansi na teknolojia ya nyuklia ni miongoni mwa taaluma za kisasa na za hali ya juu kabisa katika zama hizi. Leo hii taaluma hii ina nafasi muhimu katika kupanua maarifa ya mwanadamu, kuboresha maisha yake na kudhibiti maumbile.
Kwa kutumia vibaya teknolojia ya nyuklia, utawala wa Kizayuni umezalisha mamia ya vichwa vya silaha za nyuklia, ambavyo vinahesabiwa kuwa tishio kubwa kwa usalama wa eneo. Zipo nchi nyingine zinazotumia teknolojia hiyo kutishia maisha ya binadamu na amani ya dunia, huku Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikiruhusu tu matumizi ya amani ya teknolojia ya nyuklia kwa mujibu wa sheria na mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu pamoja na maagizo ya kiongozi wa juu kabisa nchini. Kutokana na juhudi kubwa zilizofanywa na wataalamu pamoja na watafiti wa ndani ya nchi katika nusu karne iliyopita, teknolojia hii imekuwa na nafasi muhimu katika kuimarisha uzalishaji wa viwanda, kilimo na vifaa vya tiba na matibabu nchini.
Matumizi ya radioisotopu katika utambuzi na matibabu ya magonjwa, matumizi ya teknolojia ya nyuklia katika uzalishaji umeme pamoja na utengenezaji wa aina mbali mbali za bidhaa za kilimo zinazostahimili madhara ya wadudu na ukame ni sehemu ndogo tu ya faida zinazotokana na teknolojia ya nyuklia.
Moja ya malengo muhimu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kuimarisha mpango wake wa nyuklia ni kuzalisha nishati ya nyuklia. Kwa kuzingatia masuala mbalimbali kama vile kupungua nishati inayotokana na visukuku, ongezeko la gharama za matumizi ya nishati hiyo katika sekta ya viwanda, uchafuzi wa mazingira na masuala mengine mengi, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haiwezi kupuuza manufaa makubwa yanayopatikana katika nishati ya nyuklia eti kwa sababu ina akiba kubwa ya rasilimali ya mafuta na gesi.
Kwa hivyo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inapaswa kutumia aina nyingine za nishati hususan nishati ya nyuklia katika kujidhaminia nishati kitaifa. Kwa hivyo, inatarajiwa kwamba sekta ya nyuklia ya nchi hii itaendelea kufuatilia malengo yake ya kudhamini nishati ya taifa kutokana na busara na miongozo sahihi ya viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu bila kujali vitisho vya maadui.