Vikwazo vya dawa dhidi ya Iran, jinai ya wazi ya Wamagharibi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i97174-vikwazo_vya_dawa_dhidi_ya_iran_jinai_ya_wazi_ya_wamagharibi
Mkuu wa Jumuiya ya Kuwahami Wagonjwa wa Thalassemia nchini Iran amesema kuwa, wagonjwa 662 wa ugonjwa huo wamefariki dunia humu nchini katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, kutokana na kukosa dawa kwa sababu ya vikwazo vya kidhalimu vya nchi za Magharibi dhidi ya wananchi wa Iran.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 09, 2023 21:53 UTC
  • Vikwazo vya dawa dhidi ya Iran, jinai ya wazi ya Wamagharibi

Mkuu wa Jumuiya ya Kuwahami Wagonjwa wa Thalassemia nchini Iran amesema kuwa, wagonjwa 662 wa ugonjwa huo wamefariki dunia humu nchini katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, kutokana na kukosa dawa kwa sababu ya vikwazo vya kidhalimu vya nchi za Magharibi dhidi ya wananchi wa Iran.

Yunes Arab amesema hayo kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Ugonjwa wa Thalassemia na kuongeza kuwa, ijapokuwa zaidi ya asilimia 80 ya dawa za wagonjwa wa thalassemia zinazalishwa ndani ya Iran, lakini baadhi ya wagonjwa ni vigumu mno kuwatibu kutokana na udhaifu wa miili yao, hivyo wanalazimika muda wote na katika umri wao wote watumie dawa zinazotoka nje ya Iran. Lakini wanashindwa kupata dawa hizo kutokana na vikwazo vya kidhulma walivyowekewa wananchi wa Iran na madola ya Magharibi yanayojilabu kutetea haki za binadamu.

Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mara kwa mara wamekuwa wakilalamikia athari mbaya za vikwazo vya kiholela na haramu vya Marekani dhidi ya wananchi wa Iran hasa wale wagonjwa wanaohitajia matibabu maalumu. Viongozi wa Iran wamekuwa wakitangaza mara kwa mara kuwa vikwazo hivyo vinapelekea kupoteza maisha watu wasio na hatia. Idadi ya wagonjwa hao wanaofariki dunia kutokana na vikwazo hivyo iliongezeka sana mwaka uliopita.

Amesema, mwaka 2018 wagonjwa 70 walifariki dunia, mwaka 2019 wagonjwa 90, mwaka 2020 wagonjwa 140 na mwaka 2021 wagonjwa 180 wa ugonjwa wa thalassemia walipoteza maisha nchini Iran kutokana na vikwazo vya madola ya Magharibi.

Hii ni katika hali ambayo Wamagharibi wakiongozwa na Marekani wanadamu kuwa eti suala la dawa kamwe halijawahi kuingizwa kwenye orodha ya vikwazo vyao dhidi ya Iran. Lakini ukweli wa mambo ni kuwa, madola hayo yameiwekea Iran vikwazo vikubwa vya benki na hivyo kuikwamisha kununua dawa kutoka nje. Matokoe ya vikwazo hivyo vya benki dhidi ya Iran ni kuingia hatarini maisha ya makumi ya maelfu ya wagonjwa wakiwemo wanaosumbuliwa na maradhi ya thalassemia, kensa na magonjwa mengine yanayohitajia dawa kutoka nje ya nchi.

 

 

Sayyid Haydar Mohammadi, Mkuu wa Shirika la Chakula na Dawa la Iran anasema: Wawakilishi wa baadhi ya mashirika yaliyowawekea vikwazo wananchi wa Iran wanatangaza kuwa, sisi hatuweki vikwazo lakini yanakataa kujibu maombi yote yanayowasilishwa na Iran kwa ajili ya kuuziwa dawa zinazohitajiwa na wagonjwa wenye maradhi hatari na sugu, na wanakataa kuiuzia dawa hizo Iran tena baada ya kuchelewa kutoa majibu kwa miezi mingi. Baadhi ya wakati hujitoa kimasomaso kwa kuiuzia Iran idadi ndogo sana ya dawa hizo ambazo hazikidhi chochote na kuutangazia ulimwengu kuwa eti hawajaiwekea vikwazo vya dawa Iran.

Wataalamu wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa katika uchunguzi wao waliashiria jinsi vikwazo vya Marekani vinavyowaathiri wananchi wa Iran. Alya Dohan, ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa anasema kuwa, wakati tunapozungumzia haki za kiafya za walimwengu; wagonjwa wa nchini Iran ndio watu wanaoathriwa zaidi na vikwazo inavyowekewa nchi hiyo.

Utendaji wa mashirika ya kimataifa ya dawa katika kukubaliana na vikwazo vya upande mmoja vya Marekani na woga wa mashirika hayo yasije yakawekewa vikwazo na serikali ya Marekani, ni miongoni mwa mambo yanayoikwamisha juuhudi za Iran za kuwadhaminia wananchi wake dawa hizo. 

Ni jambo lililo wazi kuwa, vikwazo vya upande mmoja vya Marekani dhidi ya Iran na vitisho vinavyotolewa na nchi hiyo kwa nchi nyingine ili zisishirikiane kivyovyote vile na Iran ikiwa ni pamoja na kuyazuia mashirika ya kigeni kushirikiana na Iran katika masuala ya tiba, afya, dawa maalumu n.k, ni mambo ambayo yana athari za moja kwa moja mbaya kwa usalama wa wananchi wa Iran na ndiyo sababu ya kupoteza maisha wagonjwa wasio na hatia nchini Iran. Huo kwa hakika ni uvunjaji wa wazi wa haki za bindamu na ni vitendo visivyo na chembe ya utu vinavyofanywa na madola ya Magharibi dhidi ya wananchi wa Iran.