Kiongozi Muadhamu: Iran inakaribisha kuhuishwa uhusiano wake na Misri
(last modified Mon, 29 May 2023 11:32:30 GMT )
May 29, 2023 11:32 UTC
  • Kiongozi Muadhamu: Iran inakaribisha kuhuishwa uhusiano wake na Misri

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema Iran inakaribisha azma ya kufufuliwa uhusiano wake na Misri.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema hayo leo katika mazungumzo yake na Sultan Haitham bin Tariq Aal Saeed wa Oman na kuongeza kuwa, "Tunakaribisha msimamo huu, na hatuoni tatizo katika (kufikiwa) hilo." 

Kiongozi Muadhamu amesema hayo baada ya kupokea ujumbe wa Misri wa kutaka kufufua uhusiano na Iran uliowasilishwa na Sultan wa Oman.

Ameipongeza serikali ya awamu ya 13 ya Jamhuri ya Kiislamu inayoongozwa na Rais Ebrahim Raisi, kwa siasa zake za nje zenye lengo la kuimarisha uhusiano na mataifa ya kieneo.

Katika mazungumzo hayo, Ayatullah Khamenei ameutaja uhusiano wa Iran na Oman kuwa wa jadi na uliokita mizizi na kubainisha kuwa, "Tunaamini kuwa, kupanuliwa uhusiano wa nchi mbili katika nyuga tofauti kutakuwa kwa maslahi ya pande mbili." 

Kiongozi Muadhamu na Sultan wa Oman

Kadhalika ameeleza bayana kuwa, kuimarishwa ushirikiano wa Tehran na Muscat kuna umuhimu mkubwa kwa kuwa nchi mbili hizi zina hisa katika mkondo wa maji wa Lango Bahari la Hormuz.

Kwengineko katika matamshi yake, Ayatullah Ali Khamenei ametahadharisha juu ya uwepo wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika eneo. "Lengo la utawala wa Kizayuni ni kuibua migawanyiko na ukosefu wa usalama katika eneo," amesema Kiongozi Muadhamu.

Kwa upande wake, Sultan Haitham bin Tariq Aal Saeed wa Oman ameeleza kuridhishwa kwake na mkutano wake na Kiongozi Muadhamu na kusema kuwa, nchi yake ina sera ya kuboresha uhusiano na majirani, haswa Jamhuri ya Kiislamu.

Sultan wa Oman akiagwa na Rais wa Iran

Sultan Haitham amesema, "Katika mazungumzo mbalimbali tuliyofanya hapa Tehran, tumejadili kuhusu kuimarisha ushirikiano katika nyuga tofauti." Amesema anatumai kwamba, kwa kuendeleza mazungumzo hayo, Iran na Oman zitaweza kupanua zaidi mahusiano yao.

Sultan wa Oman ameondoka nchini baada ya kuonana na Kiongozi Muadhamu. Alikuwa ameandamana na ujumbe wa ngazi za juu katika ziara hiyo rasmi ya siku mbili hapa Tehran.