SEPAH: Silaha za Iran ni silaha za kumsambaratisha adui + Video
(last modified Tue, 06 Jun 2023 10:01:16 GMT )
Jun 06, 2023 10:01 UTC

Kamanda wa Kikosi cha Anga za Mbali cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) amesema katika mahojiano aliyofanyiwa na shirika la habari la Iran Press wakati wa uzinduzi wa kombora la Hypersonic lililopewa jina la 'Fattah' kwamba, silaha za Iran ni za kumsambaratisha adui.

Kombora la Hypersonic la Fattah limetengenezwa na wataalamu wenyewe wa ndani ya Iran katika Kikosi cha Anga za Mbali cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH na limezinduliwa rasmi leo Jumanne katika sherehe zilizohudhuriwa na Rais Ebrahim Raisi na makamanda mbalimbali wa kijeshi, akiwemo Meja Jenerali Hossein Salami mkuu wa jeshi la SEPAH na Brigedia Jenerali Amir Ali Hajizadeh, Kamanda wa Kikosi cha Anga za Mbali cha jeshi hilo.

Akihojiwa na Iran Press, Brigedia Jeneali Hajizadeh amesema, kombora la Fattah haliwezi kutunguliwa na kombora lolote lile kama ambavyo pia haliwezi kuonekana kwenye na jambo hilo linaipa kinga kubwa Jamhuri ya Kiislamu na wananchi wa Iran. 

Brigedia Jenerali Amir Ali Hajizadeh, Kamanda wa Kikosi cha Anga za Mbali cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH

 

Kwa mujibu wa Brigedia Jenerali Amir Ali Hajizadeh, Kamanda wa Kikosi cha Anga za Mbali cha SEPAH, kombora hilo jipya la balestiki la Hypersonic la Iran, mbali na kuwa na uwezo wa kupenya kwenye mifumo ya kisasa ya kutungua makombora, lina uwezo mkubwa pia wa kupiga shabaha kwa usahihi wa hali ya juu.

Duru za kijeshi zinaarifu kuwa, makombora ya Hypersonic yana kasi mara tano zaidi ya mwendo wa sauti, na hivyo kuyapa uwezo wa aina yake ya kutoweza kuyatungua.

Kombora la balistiki la Fattah la Iran limezinduliwa siku chache baada ya kuzinduliwa rasmi kombora la Khorramshahr 4 lililopewa jina la 'Khaibar' na hizo ni miongoni mwa silaha mpya kabisa za makombora yaliyoundwa na sekta ya viwanda vya Wizara ya Ulinzi ya Iran.