Iran: Mapuuza ya Magharibi yameshadidisha mgogoro wa wakimbizi
(last modified Wed, 21 Jun 2023 03:44:29 GMT )
Jun 21, 2023 03:44 UTC
  • Iran: Mapuuza ya Magharibi yameshadidisha mgogoro wa wakimbizi

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Magharibi inajaribu kukwepa kubeba dhima ya mgogoro wa wakimbizi unaoshuhudiwa hivi sasa, na kwamba sera mbovu za Marekani na nchi za Ulaya ndizo zinazofaa kulaumiwa kwa mgogoro huo.

Nasser Kan’ani alisema hayo jana Jumanne katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter, kufuatia ajali ya kuzama kwa boti iliyokuwa imebeba wahamiaji 750 katika Bahari ya Mediterrania.

Inaarifiwa kuwa, uzembe wa mamlaka ya Ugiriki na jaribio la walinzi wake wa pwani kuilazimisha mashua hiyo ya uvuvi kuelekea kwenye maji ya eneo la Italia ndiyo sababu ya kutokea ajali hiyo iliyoua makumi ya watu.

Kan'ani amesema, "Kuzama kwa boti hiyo iliyokuwa na mamia ya wahamiaji wakiwemo wanawake na watoto kutoka nchi tofauti za Asia na Afrika katika Pwani ya Ugiriki katika maji ya Bahari ya Mediterrania ni tukio chungu la kuumiza na kusikitisha."

Kadhalika Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni wa Iran ametoa wito kwa jamii ya kimataifa kuchukua hatua madhubuti dhidi ya wasafirishaji na wanaofanya biashara haramu ya magendo ya binadamu.

Kauli ya Kan'ani imekuja siku chache baada ya Msemaji wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR), Matthew Saltmars kusisitiza umuhimu wa kuchunguza uwezekano wa kuwepo uzembe katika janga lililopelekea kuzama mashua ya wahamiaji siku ya Jumatano kwenye Rasi ya Mora ya Ugiriki, ambayo imesababisha vifo vya watu 81 na wengine 500 kutoweka. Ni wahajiri 104 pekee waliokolewa mpaka sasa.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu inatoa mkono wa pole kwa jamaa za wahanga wa ajali hiyo, akisisitiza kuwa Wamagharibi hawapasi kuendelea kupuuza na kutowajibikia mgogoro wa wakimbizi na wahamiaji.