Abdollahian amaliza safari yake ya Ghuba ya Uajemi 'kwa habari nzuri sana'
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amehitimisha safari yake ya siku tatu katika nchi jirani za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi, akisema safari hiyo itakuwa na "habari njema" kwa nchi husika na eneo zima kwa ujumla.
Hossein Amir-Abdollahian Alkhamisi alitembelea Umoja wa Falme za Kiarabu au Imarati, ambapo alijadili na kubadilishana mawazo na Rais Sheikh Mohammed bin Zayed Al Nahyan wa nchi hiyo huko Abu Dhabi kuhusu uhusiano wa nchi mbili na njia za kuimarisha ushirikiano.
Amir-Abdollahian ametoa mwaliko wa Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa Sheikh Mohammed kwa ajili ya kuitembelea Iran.
Baadaye alikutana na waziri mwenzake wa Imarati, Sheikh Abdullah bin Zayed, ambaye alisisitiza juu ya kuzingatiwa umuhimu wa mfumo wa kimataifa katika uimarishaji ushirikiano.
Wanadiplomasia hao wawili wakuu wamesisitiza umuhimu wa kukuza ushirikiano wa pande mbili hasa katika nyanja za maendeleo ya kikanda na upanuzi wa mahusiano ya nchi mbili.
Ushirikiano wa Iran na Imarati katika nyanja mbalimbali za kisiasa, kiuchumi, kibiashara, kibalozi, kiutamaduni na kisayansi ni miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa.
Safari hiyo imefanyika baada ya Abdollahian kuzitembelea nchi za Qatar, Kuwait na Oman ikiwa ni katika msururu wa hatua za karibuni zaidi za kidiplomasia za Tehran katika kuboresha uhusiano na majirani zake na vile vile kulinda usalama wa Ghuba ya Uajemi.
Kuhusiana na safari hiyo Abdollahian amesema: 'Ushirikiano kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na nchi za pwani ya kusini ya Ghuba ya Uajemi umeingia katika ukurasa mpya. Katika kila moja ya nchi hizi, tumeyapa uzito masuala ya pande mbili kwenye ajenda yetu."
Makubaliano ya Iran na Saudi Arabia mwezi Machi uliopita kwa ajili ya kurejesha uhusiano baada ya kuvunjika kwa muda mrefu yameleta mabadiliko makubwa katika ushirikiano wa kieneo na kutoa msukumo wa kutatuliwa tofauti za nchi za eneo.
Waziri huyo amesema mkutano wa kwanza wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi nane jirani, yaani zile za kusini mwa mwambao wa Ghuba ya Uajemi pamoja na Iran na Iraq, utafanyika mwezi Septemba kwa msingi wa mpango wa Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.
Katika safari hiyo Iran na Imarati pia zimetiliana saini makubaliano ya kupanua huduma za usafiri wa anga na kuongeza fursa za biashara na utalii kati ya pande mbili.