Amir -Abdollahian: Iran imependekeza ufumbuzi wa kisiasa kwa mgogoro wa Ukraine
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i99198-amir_abdollahian_iran_imependekeza_ufumbuzi_wa_kisiasa_kwa_mgogoro_wa_ukraine
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuhusu msimamo wa Iran mkabala wa vita huko Ukraine kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inapinga vita na imependekeza ufumbuzi wa kisiasa kwa mgogoro huo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 25, 2023 08:13 UTC
  • Amir -Abdollahian: Iran imependekeza ufumbuzi wa kisiasa kwa mgogoro wa Ukraine

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuhusu msimamo wa Iran mkabala wa vita huko Ukraine kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inapinga vita na imependekeza ufumbuzi wa kisiasa kwa mgogoro huo.

Imepita zaidi ya miezi 16 sasa tangu kuanza vita huko Ukraine; vita ambavyo nchi za Ulaya na Magharibi na hasa Marekani kwa kushadidisha mashinikizo na vikwazo dhidi ya Russia huku zikiipatia Kiev aina mbalimbali za silaha nyepesi na nzito si tu hazijachukua hatua yoyote ya kuhitimisha vita hivyo bali zimeendelea kuchochea moto wa mapigano nchini humo. 

Silaha za Magharibi kwa Kiev

Kuhusiana na hilo, tokea kuanza vita hivyo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikisisitiza kuwa inapinga vita vyovyote popote pale duniani na kutilia mkazo kupatiwa ufumbuzi hitilafu baina ya Russia na Ukraine kwa njia ya kisiasa; jambo ambalo limejadiliwa pia katika mazungumzo ya Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Denmark.  

Hossein Amir- Abdollahian Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na mwenzake wa Denmark, Lars Lokke Rasmussen wamezungumza kwa njia ya simu ambapo wamebadilishana mawazo kuhusu suala la kupanua ushirikiano wa pande mbili na kimataifa na pia kuhusu kadhia ya Ukraine. 

Kuhusu msimamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mkabala wa vita huko Ukraine, Amir-Abdollahian amesema: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inapinga vita na tayari imependekeza utatuzi wa kisiasa wa mgogoro wa nchi hiyo. Amesema, Iran inaamini kuwa hatua ya kuupatia silaha upande mmoja vitani itashadidisha tu mivutano na kupunguza hali ya uthabiti katika eneo. 

Katika sehemu nyingine ya mazungumzo yake na Waziri mwenzake wa Mambo ya Nje wa Denmar, Hossein Amir- Abdollahian ameutaja uhusiano wa kihistoria wa nchi mbili kuwa mtaji wenye thamani kubwa kwa ajili ya Tehran na Copenhagen na kusisitiza juu ya udharura wa kuendelezwa mazungumzo kwa ajili ya ustawi wa pande mbili. 

Katika mazungumzo hayo ya simu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Denmark pia ameutaja uhusiano wa nchi mbili hizi kuwa muhimu kihistoria, na akasema mazungumzo kati ya nchi yake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni yenye  umuhimu. Lars Lokke Rasmussen amesisitiza pia kuendelezwa ubunifu kwa ajili ya kuimarisha uhusiano wa pande mbili katika nyanja mbalimbali. 

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Denmark pia wamekubaliana kuanzisha utaratibu wa kuimarisha mashauriano ya kisiasa na kibalozi kati ya nchi mbili.