Kiongozi Muadhamu: Umoja na Umaanawi unakabiliwa na uadui na ukwamishaji wa mabeberu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i99252-kiongozi_muadhamu_umoja_na_umaanawi_unakabiliwa_na_uadui_na_ukwamishaji_wa_mabeberu
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa ujumbe muhimu kwa mnasaba wa msimu wa mwaka huu wa Hija akisema, umoja na umaanawi hivi sasa unakabiliwa na uadui na ukwamishaji mkubwa zaidi wa ubeberu, uistikbari na uzayuni.
(last modified 2026-06-17T03:32:54+00:00 )
Jun 27, 2023 04:07 UTC
  • Kiongozi Muadhamu: Umoja na Umaanawi unakabiliwa na uadui na ukwamishaji wa mabeberu

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa ujumbe muhimu kwa mnasaba wa msimu wa mwaka huu wa Hija akisema, umoja na umaanawi hivi sasa unakabiliwa na uadui na ukwamishaji mkubwa zaidi wa ubeberu, uistikbari na uzayuni.

Katika ujumbe wake huo, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amegusia kwamba, sharti la lazima la kuweza Hijja kuwa na taathira za kimataifa, ni umma wa Kiislamu kuwa na welewa sahihi wa ujumbe muhimu mno uliomo kwenye ibada hiyo ya faradhi chini ya nguzo mbili kuu za umoja na umaanawi. Amesisitiza kuwa: Marekani na kambi nyingine za mabeberu zinapinga vikali kuweko umoja kati ya Waislamu na maelewano kati ya mataifa, nchi na tawala za Waislamu kama ambavyo zinapinga vikali pia kuona vijana wa mataifa ya dunia wanafanya haraka kushikamana na mafundisho ya dini.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, maana ya umoja wa umma wa Kiislamu ni kuweko mazungumzo, kuweko mahusiano ya kifikra na kielimu, kusaidiana na kukurubiana kimkakati, kushirikiana; na nchi za Kiislamu kuwa mshikamano mzuri wa kiuchumi baina yao. Amesema, maana nyingine ya umoja wa umma wa Kiislamu ni kuweko mazungumzo baina ya maulamaa wa madhehebu tofauti ya Kiislamu kwa nia njema, kwa kuvumiliana, kwa insafu na kuweko mawasiliano ya karibu sana baina ya maulamaa na watu wenye vipaji na ushawishi katika nchi za Waislamu.

Ayatullah Khamenei amekumbushia nukta nyingine muhimu kuhusu umoja wa umma wa Kiislamu ambayo ni wajibu wa viongozi wa kisiasa na kiutamaduni wa nchi za Kiislamu kuwa na uratibu wa pamoja na kujiandaa kwa ajili ya mfumo mpya wa dunia unaokuja, ili umma wa Kiislamu uweze kuwa na nafasi yake bora unayostahiki kuwa nayo na kuzuia kujirudia uzoefu mchungu wa uhandisi wa kisiasa na kiutawala wa baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, umaanawi na masuala ya kiroho ni nguzo nyingine kati ya nguzo mbili kuu za ibada tukufu ya Hija. Maana ya nguzo hiyo ni kupandisha juu misingi ya maadili mema ya kidini na kupambana na ongezeko la maadili yanayopinga dini. Amesema, kwa muda mrefu maadili yanayopinga dini yamepandikizwa na kuenezwa na watu wa Magharibi na matokeo yake ni hivi tunavyoona leo jinsi jamii ya Magharibi ilivyoporomoka vibaya mno na hilo linashuhudiwa na kila mtu duniani.

Ayatullah Khamenei amesisitiza pia kuwa, jukumu la kila mtu na la mataifa na tawala zote ni kusimama kidete kupambana na njama za kikhabithi za Marekani na Uzayuni.