Ayatullah Khamenei: Idara ya Mahakama ilinde haki za wananchi
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza umuhimu wa kipekee wa Idara ya Mahakama ya Iran, akitaja utekelezaji kamili wa hati ya mabadiliko ya Mfumo wa Mahakama, mapambano dhidi ya ufisadi ndani na nje ya idara hiyo, kurejesha haki za umma, kudhamini uhuru halali, na kuzuia uhalifu kuwa ni miongoni mwa majukumu muhimu ya Mahakama.
Ayatullah Ali Khamenei ameyasema hayo katika kikao chake na mkuu, maafisa na wafanyakazi wa Idara ya Mahakama ya Iran, na kusisitiza kuwa majukumu ya idara hiyo kwa mujibu wa Katiba, ikiwa ni pamoja na kutekeleza haki za umma, yana umuhimu mkubwa sana. Ameongeza kuwa: Kuzuia vitisho na aina zote za uvurugaji wa usalama wa kiakili wa wananchi katika anga ya mitandao ya kijamii ni miongoni mwa madhihirisho ya kulinda haki za umma, na Idara ya Mahakama inalazimika kutekeleza wadhifa huo mgumu kwa mipango mizuri, nidhamu na kwa mujibu wa sheria.
Ayatullah Khamenei vilevile amekutaja kudhamini uhuru halali wa wananchi kuwa ni jambo muhimu na akaongeza kuwa: Kwa kuzingatia tafsiri makini ya Katiba, uhuru wote unaoruhusiwa na Sharia lazima utolewe kwa watu, na kwa kawaida taasisi za madaraka hupinga uhuru huo; hivyo Mahakama inapaswa kutimiza wajibu wake katika uwanja huu.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Idadi kubwa ya majaji na wafanyakazi wa Mahakama za Iran ni watu sharifu wanaofanya kazi ngumu zaidi kwa kipato cha chini kabisa, lakini unyanyasaji wa wachache miongoni mwao katika sehemu yoyote ya nchi unachafua sura ya Idara ya Mahakama; hivyo ufisadi wowote ndani ya taasisi hiyo unapaswa kushughulikiwa kwa umakini.