Raisi: Iran na Qatar zina suhula nzuri za kupanua ushirikiano
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i99288-raisi_iran_na_qatar_zina_suhula_nzuri_za_kupanua_ushirikiano
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezungumza kwa simu na Amir wa Qatar na kusema: Iran na Qatar zina suhula nzuri za kupanua ushirikiano wao wa pande mbili, wa kikanda na kimataifa.
(last modified 2026-06-17T03:32:54+00:00 )
Jun 28, 2023 04:39 UTC
  • Raisi: Iran na Qatar zina suhula nzuri za kupanua ushirikiano

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezungumza kwa simu na Amir wa Qatar na kusema: Iran na Qatar zina suhula nzuri za kupanua ushirikiano wao wa pande mbili, wa kikanda na kimataifa.

Rais Sayyid Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amejibu wito wa simu ya Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani Amir wa Qatar ambapo amempongeza yeye na wananchi wa Qatar kwa kuwadia Sikukuu ya Idul Adh'ha na kusema: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikitilia mkazo kuimarisha uhusiano na kupanua ushirikiano kati yake na Qatar. 

Rais Raisi amemshukuru Amir na Waziri Mkuu wa Qatar kwa jitihada zao za kufanikisha mipango na mapatano ya pamoja na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuongeza kuwa, Iran inaamini kuwa kuendelezwa uhusiano wa pande mbili kutapelekea kuboreshwa zaidi ushirikiano wa kikanda na kimataifa kati ya pande mbili.  

Katika mazungumzo hayo ya simu, Amir wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani ametoa mkono wake wa kheri na fanaka kwa Rais na wananchi wa Iran kwa mnasaba wa Sikukuu ya Idul- Adh'ha na akasema: Nchi yake ipo tayari kuzidisha kiwango cha ushirikiano wa kiuchumi na uwekezaji na Iran na kwamba kwa kuzingatia mazungumzo na majadiliano mazuri yaliyofanywa kuhusu kustawisha uhusiano wa pande mbili, Qatar na Iran ziko tayari kuitisha mkutano wa Kamisheni ya Pamoja ya Ushirikiano wa Kiuchumi siku chache zijazo.  

 Uhusiano wa Iran na Qatar ni miongoni mwa uhusiano thabiti na wa kirafiki katika eneo la Asia Magharibi, ambao umekumbwa na misukosuko kwa kiwango kidogo.