Iran yayaasa mataifa ya Waislamu kuungana kuzima njama za maadui
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i99344-iran_yayaasa_mataifa_ya_waislamu_kuungana_kuzima_njama_za_maadui
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Iran ametoa mwito kwa mataifa ya Kiislamu kuwa na umoja na mshikamano mkabala wa njama za maadui na lobi za Kizayuni, zenye azma ya kuibua mifarakano na ukosefu wa uthabiti katika nchi hizo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jun 30, 2023 03:25 UTC
  • Iran yayaasa mataifa ya Waislamu kuungana kuzima njama za maadui

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Iran ametoa mwito kwa mataifa ya Kiislamu kuwa na umoja na mshikamano mkabala wa njama za maadui na lobi za Kizayuni, zenye azma ya kuibua mifarakano na ukosefu wa uthabiti katika nchi hizo.

Hossein Amir-Abdollahian alitoa mwito huo jana Alkhamisi hapa mjini Tehran katika mkutano wake na mabalozi, mabalozi wadogo na wakuu wa ofisi za kibalozi wa nchi za Kiislamu hapa nchini Iran, kwa mnasaba wa sikukuu ya Iddul Adh'ha.

Amebainisha kuwa, maadui wa umma wa Kiislamu wamepanga njama za kuyagawa mataifa ya Kiislamu ili kuyadhoofisha. Amir-Abdollahian amesisitiza kuwa, "Juhudi zetu za pamoja zinapasa kuelekezwa katika kuvunja njama za maadui wa Uislamu na lobi za Kizayuni zinazotaka kuibua mgawanyiko miongoni mwa mataifa ya Waislamu ikiwemo Sudan."

Amesema kwamba, kwa mshikamano na kudumisha umoja, ulimwengu wa Kiislamu utaweza kusambaratisha njama za maadui wasiweze kufikia malengo yao kama walivyofeli huko nyuma katika nchi za Afghanistan, Syria, na Iraq.

Baadhi ya mataifa ya Kiislamu yaliswali Swala ya Iddul Adh'ha jana Alkhamisi

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran amesema uhusiano wa Iran na Misri na Moroco utafufuliwa kikamilifu kutokana na siasa za nje za serikali ya 13 ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu inakaribisha azma ya kuimarishwa na kupanuliwa uhusiano na ushirikiano wake na mataifa ya Kiislamu yakiwemo Misri na Morocco.

Kadhalika Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amebainisha kuwa, Palestina itaendelea kuwa kadhia kuu ya Ulimwengu wa Kiislamu, na kwamba Waislamu wanapasa kuwa macho na kusimama kidete dhidi ya jinai za Wazayuni kwa Wapalestina.