Iran: Aliyechoma moto Qurani Sweden ana uhusiano na MOSSAD
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i99778-iran_aliyechoma_moto_qurani_sweden_ana_uhusiano_na_mossad
Wizara ya Intelijensia ya Iran imefichua mfungamano uliopo baina ya Salwan Momika, raia wa Sweden aliyechoma moto nakala ya Qur'ani Tukufu mjini Stockholm mwezi uliopita na shirika la ujasusi la Israeli (MOSSAD).
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 11, 2023 04:10 UTC
  • Iran: Aliyechoma moto Qurani Sweden ana uhusiano na MOSSAD

Wizara ya Intelijensia ya Iran imefichua mfungamano uliopo baina ya Salwan Momika, raia wa Sweden aliyechoma moto nakala ya Qur'ani Tukufu mjini Stockholm mwezi uliopita na shirika la ujasusi la Israeli (MOSSAD).

Taarifa iliyotolewa jana Jumatatu na wizara hiyo imeeleza kuwa, kitendo hicho cha kukivunjia heshima Kitabu kitukufu cha Waislamu nchini Sweden kilikusudia kupotosha fikra za waliowengi duniani ili wasishughulishwe na jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina hasa mjini Jenin katika eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Duru za kuaminika zimeiambia Wizara ya Intelijensia ya Iran kuwa, Salwan Momika ambaye alizaliwa nchini Iraq mwaka 1986, alijiunga na shirika la ujasusi la Israeli (MOSSAD) mwaka 2019.

Inaarifiwa kuwa, alipokuwa Iraq, aliyafanyia ujasusi makundi ya muqawama kwa maslahi na Israel na kusababisha kuyumba kwa uthabiti katika nchi hiyo ya Kiarabu.

Wizara ya Intelijensia ya Iran imesema utawala wa Kizayuni ilihakikisha Momika anapata uraia wa Sweden, kama zawadi ya kulisaliti taifa la Iraq na umma wa Kiislamu kwa kuwa jasusi wake.

Momika, ajenti wa MOSSAD aliyechoma moto Qurani Sweden

Juni 28, Momika mwenye umri wa miaka 37, alichoma moto nakala ya Qur'ani Tukufu mbele ya Msikiti mkuu wa Stockholm, siku ambayo Waislamu Sweden walikuwa katika siku ya kwanza ya Idul Adh’ha.

Mkimbizi huyo wa Iraq aliyepewa uraia wa Sweden alikivunjia heshima Kitabu kitakatifu cha Waislamu bilioni mbili kwa kibali cha mahakama ya Sweden na kwa ulinzi kamili wa jeshi la polisi la nchi hiyo ya Ulaya Magharibi.

Waislamu kote duniani wameendelea kupaza sauti zao kulaani kitendo hicho kiovu cha kudhalilisha na kuvunjiwa heshima Qurani Tukufu nchini Sweden, huku kampeni kubwa ya dunia nzima ya kususia bidhaa zinazozalishwa na nchi hiyo ya Magharibi ikishika kasi.