Zimbabwe, kituo cha mwisho cha safari ya Rais wa Iran barani Afrika
Rais Ibrahim Rais wa Jamhuri ya Kiislamu jana Alkhamisi aliwasili Harare mji mkuu wa Zimbabwe ambapo alikutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa nchi hiyo akiwemo mwenyeji wake, Rais Emerson Mnangagwa.
Zimbabwe ni kituo cha tatu na cha mwisho cha safari ya kiduru ya Rais Ebrahim Rais barani Afrika ambapo kabla ya hapo alizitembea Kenya na Uganda zilizozoko katika Ukanda wa Afrika Mashariki. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, daima bara la Afrika limekuwa likipewa kipaumbele katika sera za kigeni za Iran. Hata hivyo baada ya Serikali ya Awamu ya 13 kuingia madarakani na kuanza rasmi kazi zake Agosti mwaka 2021 chini ya uongozi wa Rias Ebrahim Raisi, kumeonekana azma thabiti ya kutaka Iran iwe na mahudhurio makubwa zaidi barani Afrika.
Katika mkondo wa sera hizo za Serikali ya Awamu ya 13, mwaka jana 2022, Hussein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu alifanya safari katika nchi za Tanzania, Mali na Mauritania. Aidha kabla ya kuanza safari yake ya kuzitembelea nchi kadhaa za Kiafrika, Rais Ebrahim Raisi alisema, lengo la safari yake ya kuzitembelea nchi hizo tatu za Kenya, Uganda na Zimbabwe ni kuitikia mwaliko rasmi wa marais wa nchi hizo na kuimarisha ushirikiano akisisitiza kuwa, bara la Afrika linapewa umuhimu mkubwa katika siasa za mambo ya nje za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Miongoni mwa nchi za Kiafrika, Zimbabwe inahesabiwa kuwa moja ya nchi ambazo zimekuwa na uhusiano wa kirafiki siku zote na Iran baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Sambamba na hayo, kuwepo uwezo na fursa nyingi za kiuchumi katika nchi hizo mbili pia kumeandaa mazingira ya kukuza na kupanua uhusiano na ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.
Katika fremu hiyo, mazungumzo ya ushirikiano wa kibiashara kati ya Iran na Zimbabwe yalifanyika mwaka jana hapa mjini Tehran wakati wa ziara ya Waziri wa Viwanda wa Zimbabwe, na hati za ushirikiano zilitiwa saini kati ya nchi hizo mbili katika mkutano wa tisa wa Kamisheni ya Pamoja.
Zimbabwe, yenye watu milioni 15, ni nchi ndogo isiyo na bahari kusini mwa bara la Afrika. Nchi hii inapakana na Msumbiji upande wa kaskazini-mashariki, mashariki na kusini-mashariki, Afrika Kusini upande wa kusini, Botswana upande wa magharibi na kusini-magharibi, na Zambia upande wa kaskazini na kaskazini-magharibi. Mji mkuu wa nchi hiyo ni Harare. Kuna lugha 16 rasmi kati ya watu wa nchi hii. Hata hivyo zinazojulikana zaidi ni Kiingereza, Kishona na Ndebele
Kilimo na madini vinachangia kwa kiasi kikubwa katika mauzo ya nje ya nchi hiyo. Zimbabwe pia ina akiba ya madini ya chromite na hifadhi nyingine za madini ikiwa ni pamoja na makaa ya mawe, asbesto, shaba, nikeli, dhahabu, platinamu na madini ya chuma.
Zimbabwe inapata pato kubwa la kila mwaka kutokana na mauzo ya tumbaku, kiasi kwamba, filihali inasafirisha tumbaku katika nchi zaidi ya 60 duniani. Katika miaka ya hivi karibuni, sekta hii imekuwa na mchango mkubwa katika kusaidia uchumi wa Zimbabwe kupitia uboreshaji wa akiba ya fedha za kigeni.
Uhusiano wa Iran na Zimbabwe tangu mwanzo wa uhuru wa nchi hiyo, umekuwa mzuri. Wapigania uhuru wa Zimbabwe walituma ujumbe wa nchi hiyo nchini Iran mwaka 1980 ambao ulikutana na kufanya mazungumzo na Imam Khomeini (RA) katika mji wa Qum, na kwa muktadha huo kukawa kumeandaliwa mazingira mazuri ya kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia baina ya pande mbili mara tu baada ya Zimbabwe kupata uhuru. Katika fremu hiyo, mwaka 1361 Hijria Shamsia, (1982) ubalozi wa Iran mjini Harare ulifunguliwa. Aidha Zimbabwe nayo ilifungua ubalozi wake mjini Tehran mwaka 2003. Baada ya Iran kufungua ubalozi mjini Harare, safari za viongozi wa pande mbili ziliongezeka
Mbali na uhusiano wa pande mbili, Iran na Zimbabwe zimekuwa na ushirikiano mzuri katika ngazi za kikanda na kimataifa katika kipindi cha miongo minne iliyopita. Katika mazingira ya baada ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kuingia madarakani serikali mpya ya Zimbabwe inayoongozwa na Rais Emmerson Mnangagwa, zimejitokeza fursa zaidi za ushirikiano wa pane mbili.
Uhusiano wa kibiashara kati ya Iran na Zimbabwe na fursa zilizojitokeza kulingana na takwimu zilizochapishwa na Idara ya Ushuru na Forodha ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, mabadilishano jumla ya biashara kati ya Iran na Zimbabwe yalipungua mwaka uliopita ikilinganishwa na mwaka wa kabla yake. Kutokana na vikwazo vya kimataifa, Zimbabwe inahitaji uwekezaji wa kigeni katika miradi ya ujenzi, na kutokana na uwezo wake wa kiuchumi, Iran inaweza kufanya kazi nchini Zimbabwe katika miradi kama vile utengenezaji wa matrekta, viwanda vya kutengeneza dawa, uhamishaji wa teknolojia na kilimo cha kuvuka mipaka.
Kwa kutilia maanani uhusiano ulio imara na usio na mivutano kati ya Iran na Zimbabwe katika miaka ya nyuma, pamoja na ukweli kwamba nchi zote mbili ziko chini ya vikwazo vya madola ya Magharibi, tunaweza kusema kuwa, matokeo ya kuongezeka kwa uhusiano wa kisiasa na kiuchumi kati ya Iran na Zimbabwe yanaweza kudhamini maslahi ya nchi hizo mbili, na kwa sababu hiyo, safari ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Zimbabwe bila shaka ni fursa ya kutambulishana uwezo wa kiuchumi na kibiashara na kutiliana saini mikataba mipya kwa lengo la kuondoa vizingiti na kupanua ushirikiano.