Feb 24, 2024 10:45 UTC
  • Hamas: Ndege za Marekani zinashiriki mauaji ya kimbari ya Israel dhidi ya Wapalestina Gaza

Afisa wa ngazi ya juu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, amesema Marekani inatumia ndege za ujasusi katika Ukanda wa Gaza ili kusaidia katika vita vya mauaji ya kimbari vinavyoendeshwa na utawala haramu wa Israel dhidi ya eneo hilo.

Akizungumza mjini Beirut, Osama Hamdan, mwakilishi mkuu wa Hamas nchini Lebanon amefichua kuwa, ndege za Marekani zinatekeleza oparesheni juu ya Gaza ili kuipa Israel taarifa za kijasusi ambazo zinaisaidia kuendelea na mashambulizi ya kijeshi.

Afisa huyo hakutaja aina ya ndege zinazotumika, lakini Marekani kwa kawaida hutumua ndege za kisasa zisizo na rubani duniani kote kukusanya taarifa za kijasusi.

Marekani imekuwa ikiiunga mkono Israel kisiasa na kijeshi katika vita vyake vya mauaji ya kimbari dhidi ya Ukanda wa Gaza tokea  Oktoba 7, 2023.

Utawala wa Marekani hadi sasa umetumia kura yake ya turufu kupinga maazimio matatu ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambayo yametaka kusitishwa mara moja kwa vita vya Israel dhidi ya Gaza.

Washington pia imeipa Tel Aviv silaha zaidi ya tani 10,000 za vifaa vya kijeshi tangu kuanza kwa vita. Hamdan alisema utawala wa Israel hautaweza kuendeleza vita -- ambavyo hadi sasa vimeua Wapalestina 29,514, wengi wao wakiwa wanawake na watoto -- bila ya kuungwa mkono na Washington.

Kwingineko katika matamshi yake, Hamdan alihimiza kufanyika kwa uchunguzi huru kuhusu ripoti ya hivi karibuni ya Umoja wa Mataifa inayofichua aina nyingi za unyanyasaji unaofanywa na wanajeshi wa Israel dhidi ya wanawake na watoto wa Kipalestina huko Gaza na Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.

Amekosoa kimya cha Wamagharibi kuhusiana na taarifa ya utawala huo kukiuka haki za wanawake wa Kipalestina waliotekwa nyara.

Mjumbe wa Hamas, wakati huo huo, alisema "utawala wa kigaidi" wa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ulikuwa unatafuta kuongeza muda wa vita ili kumsaidia Waziri Mkuu kuepuka matatizo yake ya kisheria. Netanyahu anashitakiwa kwa tuhuma za hongo, ulaghai na uvunjaji wa uaminifu.