Ulimwengu wa Michezo, Jan 26
https://parstoday.ir/sw/news/event-i135918-ulimwengu_wa_michezo_jan_26
Hujambo msikilizaji mpenzi, na karibu tutupie jicho baadhi ya matukio makubwa ya spoti yaliyojiri ndani ya siku zilizopita kote duniani.
(last modified 2026-02-10T07:17:34+00:00 )
Jan 26, 2026 09:18 UTC
  • Ulimwengu wa Michezo, Jan 26

Hujambo msikilizaji mpenzi, na karibu tutupie jicho baadhi ya matukio makubwa ya spoti yaliyojiri ndani ya siku zilizopita kote duniani.

Tenisi: Muirani ang'ara

Benyamin Faraji, bingwa wa tenisi wa Iran ametwaa taji katika Mashindano Dunia ya Tenisi ya Mezani ya Vijana ya WTT Doha 2026 nchini Qatar. Faraji alimchakaza Man Long wa Hong Kong na kumshinda kwa seti 3-0 katika safu ya vijana wa kiume wenye chini ya miaka 17.

 

Kabla ya pambano la fainali, aliwapeleka mchaka mchaka wachezaji bingwa wa tenisi kutoka India, Malaysia, na Korea Kusini. Arshia Lorestani, mwakilishi mwingine wa Iran katika mashindano hayo ya tenisi ya dunia, alishindwa kusonga mbele hadi Raundi ya Nane. Mashindano hayo ni muhimu katika mfululizo mpana wa Tenisi ya Mezani ya Kimataifa ya Qatar. Mashindano hayo ya kimataifa ya tenisi ya vijana yalifikia tamati Jumapili ya Januari 25.

Handiboli; Iran yainyuka Australia

Timu ya handiboli ya Iran iliigaragaza Australia 39-13 kwenye Mashindano ya 22 ya Mpira wa Mikono ya Wanaume wa Asia siku ya Jumamosi. Iran, ambayo ilipoteza dhidi ya Saudi Arabia kwa alama 24-22 katika mechi yao ya ufunguzi, iliishinda India 39-16 katika Kundi la 4 la mashindano hayo ya Asia ya 2026 siku ya Alkhamisi. Mashindano hayo ya kibara yaliyoanza Januari 15, yanatazamiwa kufikia kileleni tarehe 29 mwezi huu wa Januari huko Sabah Al-Salem, nchini Kuwait.

 

Timu mbili bora kutoka kila kundi zitasonga mbele hadi raundi kuu, ambayo itazishirikisha timu nane zilizogawanywa katika makundi mawili. Timu mbili bora kutoka kila kundi zitafuzu kwa hatua ya nusu fainali, pamoja na kujikatia tiketi ya moja kwa moja ya Mashindano ya Dunia ya Handiboli 2027. Qatar ndiyo mabingwa watetezi wa kombe hilo.

Ligi Kuu Iran; Persepolis kileleni

Klabu ya soka ya Persepolis iliigaraza Sepahan mabao 2-1 katika mechi ya wiki ya 17 ya Ligi Kuu ya Soka ya Iran siku ya Ijumaa na kutuama kileleni mwa jedwali la ligi hiyo inayofahamika kama Persian Gulf Pro League (PGPL) wakiwa na alama 31. Katika mchezo huo uliopigwa katika uwanja uliojaa theluji, Oston Urunov aliwaweka kifua mbele wenyeji kwa kutikisa nyavu kunako dakika ya 53 ya mchezo, huku Ivan Sergeev akifanya mambo kuwa mabao 2-0 katika dakika ya 72. Ricardo Alves alifunga bao la kufutia machozi la Sepahan walioko katika nafasi ya pili jedwalini, katika dakika za lala salama. Baadaye siku hiyo, Esteghlal na Zob Ahan zilitoa sare tasa huko Isfahan. Katika mechi nyinginezo, Gol Gohar iliwashinda Fajr Sepasi mabao 2-0, Esteghlal Khuzestan walitoshana nguvu na Paykan kwa kutoa sare tasa, huku Chadormalou na Shams Azar Tabriz wakigawana pointi katika sare ya 0-0.

 

Persepolis ilipanda kileleni kwa pointi 31, kutokana na tofauti kubwa ya mabao kuliko Sepahan ambapo pia wana alama 31. Teractor Sazi au ukipenda waite wazalishaji wa matrekta wa Iran wanafunga mduara wa tatu bora ligini kwa sasa wakiwa na pointi 29.

Soka Afrika; Simba, Yanga walazwa na Waarabu

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga SC, walikubali kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya Al Ahly ya Misri katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika uliopigwa Ijumaa ya Januari 23, katika Uwanja wa Borg El Arab, nchini Misri. Zikiwa zimesalia sekunde chache kabla ya timu hizo kwenda mapumzikoni, nyota wa Al Ahly, Mahmoud Trezeguet, alifunga bao la kwanza na kuwapa wenyeji uongozi.

 

Kipindi cha pili, dakika ya 75, Trezeguet aliongeza bao la pili ambalo lilibaki mpaka mwisho wa mchezo, na kuwapa ushindi Waarabu hao wa Afrika Kaskazini, dhidi ya 'Wananchi' kutoka Afrika Mashariki. Kufuatia matokeo hayo, Al Ahly wanaongoza Kundi B wakiwa na pointi 7, wakifuatiwa na Yanga wenye pointi 4 baada ya kucheza michezo mitatu. Timu nyingine za Waarabu za AS FAR na Kabylie zina pointi 1 kila moja, zikiwa zimecheza michezo miwili.

Wakati huo huo, klabu ya Simba SC ya Tanzania imeendeleza rekodi ya kupoteza kwenye michuano hiyo ya Champions League ya Shirikisho la Soka Afrika CAF. Hii ni baada ya kufungwa bao 1-0 na Esperance De Tunis na kuendelea kuvuta mkia kwenye Kundi D ikiwa haina pointi. Simba hawajavuna alama yeyote mpaka sasa kwenye mashindano ya CAF CL, na unaweza kusema ndiyo timu yenye matokeo mabaya zaidi kwenye mashindano hayo mpaka sasa. Kwenye michezo yake miwili iliyopita, Simba ilifungwa bao 1-0 na Petro de Luanda katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kabla ya kufungwa mabao 2-1 na Stade Malien ya Mali ugenini.

 

Esperance ilitoka sare na Petro de Luanda ya Angola na Stade Malien ya Mali. Simba itarudiana na Esperance wiki ijayo katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, na ili wafuzu hatua ya robo fainali wanatakiwa washinde michezo yao yote iliyobaki huku wakiwaombea mabaya wapinzani wao. Yanga SC inatarajiwa kusafiri kwenda Zanzibar kwa ajili ya kambi maalum ya maandalizi kuelekea mchezo mkubwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly ya Misri, utakaochezwa tarehe 31 Januari. Katika mchuano mwingine wa kusisimua wa Ligi ya Klabu Bingwa Afrika, Mamelodi Sundown ya Afrika Kusini ililazimishwa sare ya mabao 2-2 na Al-Hilal ya Sudan.

Huku hayo yakiarifiwa, klabu ya Azam ya Tanzania imezima matumaini ya klabu ya Nairobi United ya kusonga mbele kwenye mashindano ya kikanda ya Kombe la Shirikisho la Afrika. Hii ni baada ya kuigaragaza klabu hiyo ya Kenya mabao 2-1 katika mchuano wa Jumapili, uliopigwa katika Uwanja wa Nyayo jijini Nairobi. Vijana wa Nairobi walishindwa kutumia vizuri fursa ya kuchezea nyumbani mbele ya makumi ya maelfu ya mashabiki, na wakajikuta wanapoteza mechi hiyo muhimu. Kulikuwa na matumaini kwamba mwenyeji angeagua ndoto zake za kutinga robo fainali baada ya kuongoza katika dakika ya 13 kwa bao lililofungwa na Duncan Omalla Odhiambo. Hata hivyo Azam walijizoa na kufanya mambo kuwa sawa bin sawa kupitia goli la Mkogomani, Jephte Kitambala dakika tatu baadaye. Azam waliikaba koo Nairobi United katika mchezo huo wa Kundi B na kuvuna bao la ushindi kunako dakika ya 78, lililohesabiwa kuwa ni la kujifunga, ingawaje shuti lenyewe lilifumwa na Himid Mao. Timu hiyo ya Kenya huko nyuma ilipoteza kwa mabao 3-0 ilipovaana na Wydad Casablanca ya Morocco, na bao 1-0 dhidi ya Maniema Union kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Aidha wikendi hii, timu ya FC Lupopo ya DRC iliitandika AC Alger ya Algeria bao moja la uchungu bila jibu katika mchuano wa Kundi C kwenye Confederation Cup.

Katika hatua nyingine, Kocha wa Senegal Pape Thiaw ametetea uamuzi wa timu yake wa kuondoka uwanjani wakati wa fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika, akisema ulikuwa uamuzi wa kihisia uliochukuliwa wakati wa machafuko ya wakati huo. "Haikuwa nia yangu kamwe kwenda kinyume na kanuni za mchezo ninaoupenda sana," Thiaw aliandika kwenye Instagram siku ya Alkhamisi. "Nilijaribu tu kuwalinda wachezaji wangu kutokana na dhuluma. Kile ambacho baadhi wanaweza kukiona kama ukiukaji wa sheria si kitu zaidi ya hisia tu kwa upendeleo wa hali hiyo. Baada ya kujadiliana, tuliamua kuendelea na mechi na kutafuta kombe."

Dondoo za Hapa na Pale

Tuanze na Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza, ambapo Manchester United iliipa kipigo Arsenal, huku bao la Matheus Cunha likiwasaidia Mashetani Wekundu kupata ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya vinara Wabeba Bunduki. Katika mchuano huo wa Jumapili uliowakutanisha watani hao wa jadi, bao la kiustadi la Patrick Dorgu liliipa United uongozi kabla bao la kusawazisha la Mikel Merino lililoonekana kuwa limeokoa pointi moja kwa Arsenal. Cunha, ambaye ni mshambuliaji mahiri kutoka Brazil Cunha alifunga bao la aina yake la ushindi dakika tatu kabla ya mechi kumalizika. Bao la kujifunga la Lisandro Martinez liliiweka Arsenal kifua mbele katika Uwanja wa Emirates siku ya Jumapili, lakini Bryan Mbeumo alisawazisha kabla ya mapumziko.

 

Gunners sasa wana pointi nne tu juu ya Manchester City walioko katika nafasi ya pili na Aston Villa walio nafasi ya tatu jedwali, ambao wote walifunga pengo kwa ushindi dhidi ya Wolves na Newcastle mtawalia, wikendi hii. Kocha wa Arsenal Mikel Arteta hajanyanyua kombe lolote tangu Kombe la FA la 2020, na Arsenal, ambayo haijashinda taji hilo kwa miaka 22, inakabiliwa na mtihani mzito katika wiki zijazo baada ya kupata uongozi muhimu kileleni katika mbio za ubingwa zilizopita.

Mbali na hayo, Iran inapanga kutuma wanariadha kati ya 300 na 350 kwenye Michezo ya Asia ya 2026 huko Nagoya nchini Japan, ingawaje hakuna orodha ya timu au wanariadha iliyopasishwa rasmi kufikia sasa. Asghar Rahimi, mjumbe mkuu wa Iran kwenye mashindano hayo ya dunia akizungumzia kuhusu mikutano inayoendelea kati ya Kamati ya Kitaifa ya Olimpiki (NOC), Wizara ya Michezo, na mashirikisho ya kitaifa, Rahimi amesema majadiliano yanaendelea kutathmini utayarifu wa timu na wanamichezo, na kufafanua vigezo vya ushiriki badala ya kushughulishwa na uteuzi wa mwisho.

Huku hayo yakiarifiwa, timu ya taifa ya mpira wa miguu ya Iran itaendeleza maandalizi yao kwa Kombe la Dunia la FIFA la 2026 kwa mchezo wa kirafiki dhidi ya Cameroon mnamo Machi 30 huko Istanbul. Mechi hiyo, iliyothibitishwa na Shirikisho la Soka la Iran, ni sehemu ya mpango mpana wa 'Team Melli' wa kukabiliana na upinzani mkali na tofauti kabla ya mashindano hayo ya dunia baadaye mwaka huu.

Kwengineko, Rais wa Shirikisho la soka la Ujerumani (DFB), amesema ni wakati wakati wa kujiondoa kwenye Kombe la Dunia la 2026 kutokana na hatua ya Rais wa Marekani Donald Trump. Marekani itakuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia msimu wa joto mwaka huu, ikishirikiana na Canada na Mexico. Mapema mwezi huu, Rais Trump aliwakasirisha viongozi wa Ulaya kuhusu azma yake ya kutwaa kisiwa cha Greenland, ambacho sasa kinasimamiwa na Denmark. Itakumbukwa kuwa Marekani iliwahi kuzihimiza nchi nyingine kususia michezo ya Olimpiki ya 1980 kwa sababu ya Muungano wa Kisovieti kuivamia Afghanistan.

Kombe la Dunia FIFA 2026

 

Wakati huo huo, kura ya maoni ya hivi karibuni iliyofanywa na Taasisi ya INSA imefichua matokeo ya kushangaza; 47% ya Wajerumani wameunga mkono wazo la kususia Kombe la Dunia FIFA 2026 iwapo Washington intanyakua eneo la Greenland, ikilinganishwa na 35% waliopinga wazo hilo.

Na Kocha mkuu wa Uturuki wa timu ya mpira wa kikapu ya Ugiriki Panathinaikos alitukanwa kabla na wakati wa mchezo wa EuroLeague Alkhamisi dhidi ya timu ya Israel ya Maccabi Rapyd Tel Aviv. Kabla ya mechi hiyo huko Tel Aviv, mashabiki wapatao 300 wa Maccabi waliokuwa wamekusanyika kwenye lango la uwanja walimtusi Ergin Ataman na klabu ya Ugiriki. Mashabiki wa Israel waliendelea kuimba matusi wakati wa mchezo na baada ya kipyenga cha mwisho huku Ataman akielekea kwenye chumba cha kubadilishia nguo. Ataman amesema kwamba, licha ya unyanyasaji huo, waamuzi na maafisa walishindwa kuingilia kati.

………………..MWISHO….………..