Moscow: Utekaji nyara wa Maduro ulifanyika kwa uhaini wa ndani
-
Askari wa Marekani wakimshikilia Maduuro
Balozi wa Russia nchini Venezuela amesema Rais wa nchi hiyo, Nicolas Maduro, alisalitiwa na vibaraka wa ndani nchini humo.
Sergey Melik-Bagdasarov, balozi wa Russia mjini Caracas, anasema anaamini inawezekana kabisa kwamba Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro, alisalitiwa na maafisa usalama na wa jeshi la nchi hiyo.
"Maafisa wengi wa jeshi, usalama na watekelezaji wa sheria hawakufanya walichopaswa kufanya. Ikiwa kilichokuwa kikiendelea hapa muda mrefu kabla ya suala hili kutokea kinaweza kuitwa uhaini, basi kwa kawaida ulikuwa uhaini," amesema Sergey Melik-Bagdasarov katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Rossiya-24.
Balozi wa Russia nchini Venezuela amesisitiza kuwa: "Tunayajua majina ya wasaliti hao waliokimbia Venezuela na kufanya kazi kimfumo kwa ajili ya taasisi za ujasusi za Marekani."
Hapo awali Gazeti la Marekani The New York Times liliripoti kwamba chanzo cha Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) ndani ya serikali ya Venezuela kilisaidia askari maalumu wa Marekani katika operesheni ya kumteka nyara Maduro.
Ikinukuu kile ilichokiita vyanzo chenye taarifa kuhusu operesheni hiyo, ripoti hiyo ilidai kwamba chanzo kimoja chenye uhusiano na Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) ndani ya serikali ya Venezuela kilikuwa kimefuatilia eneo la Rais wa Venezuela Nicolas Maduro katika siku na muda mfupi kabla ya askari maalumu wa operesheni ya Marekani kumteka nyara.