Iran yazifungulia mashitaka US, Israel kwa kuunga mkono ugaidi
Iran imewasilisha malalamiko ya kisheria na jinai katika majukwaa ya kimataifa dhidi ya Marekani, utawala wa Kizayuni wa Israel, na makundi kadhaa ya kigaidi kwa kuunga mkono na kufadhili vitendo vya ugaidi na uhaini dhidi ya usalama wa taifa wa Iran.
Washtakiwa hao wamehusika katika kuunga mkono shughuli za kuvuruga utulivu na vitendo vya hujuma vilivyolenga kudhoofisha usalama wa nchi.
Machafuko yaliyochochewa na maajinabi nchini Iran yalipamba moto Januari 8 na kuendelea kwa siku kadhaa, kufuatia maandamano ya amani katika masoko ya Iran ambapo wafanyabiashara walikuwa wanalalamikia kushuka kwa thamani ya sarafu ya Iran.
Ghasia hizo, zilizochochewa waziwazi na utawala wa Israel na Rais wa Marekani Donald Trump, zilisababisha uharibifu mkubwa wa mali za umma na za kibinafsi, pamoja na uharibifu mkubwa wa maduka, taasisi za serikali, vifaa vya huduma za umma, na mauaji ya maelfu ya raia, wakiwemo wanawake na watoto, pamoja na maafisa usalama.
Mamlaka za Iran zimethibitisha kwamba, mashirika ya ujasusi ya Marekani na Israel yalihusika moja kwa moja, yakitoa ufadhili, mafunzo, na usaidizi wa vyombo vya habari kwa wafanya ghasia na magaidi waliokuwa na silaha.
Mkuu wa Idaya ya Mahakama ya Iran, Gholam-Hossein Mohseni-Eje’i amesema kwamba, Marekani na Israel ndio mawakala wakuu nyuma ya ghasia za hivi karibuni, akibainisha kwamba walikuwa na jukumu la moja kwa moja na la wazi katika matukio hayo, badala ya kujiwekea kikomo cha usaidizi usio wa moja kwa moja.
Katika mkutano uliofanyika ili kufuatilia mchakato wa mahakama katika kesi za wale waliohusika katika ghasia za hivi karibuni, amesema kwamba, wakati wa ghasia za hivi karibuni, "Marekani mtenda jinai" na "utawala wa Kizayuni" zilitoa waziwazi msaada wa kifedha, kijeshi, na mafunzo kwa magaidi na wafanya fujo, akiongeza kwamba machafuko ya karibuni ni muendelezo na awamu nyingine ya vita vya siku 12.