Apr 11, 2024 02:27 UTC
  • Waislamu wa Ghaza wasali Sala ya Idi juu ya vifusi, maelfu wasali Idi katika Msikiti wa al Aqsa

Waislamu wa Ukanda wa Ghaza jana Jumatano walitekeleza ibada ya Sala ya Idul Fitr juu ya vifusivya Misikiti na shule zilizobomolewa kikatili na utawala wa Kizayuni huku maelfu ya Waislamu wa Palestina wakitekeleza ibada hiyo kwenye Msikiti wa al Aqsa katika mji mtakatifu wa Baytul Muqaddas.

Shirika la habari la IRNA limeripoti kuwa Waislamu wa Palestina wa mji wa Rafah wa kusini mwa Ukanda wa Ghaza wametekeleza ibada ya Sala ya Idul Fitr juu ya mabaki ya Misikiti na shule zilizobomolewa katika mashambulizi ya kinyama ya wanajeshi makatili wa Israel. 

Huko Khan Yunis, makumi ya Waislamu wa mji huo wa kusini mwa Ghaza nao wametekeleza ibada ya Sala ya Idi ndani ya hospitali kutokana na mji kuharibiwa vibaya na mabomu na makombora ya wanajeshi wa utawala wa Kizayuni.

Waislamu wa Palestina wanashiriki kwa maelfu kwenye Sala za Idi na Ijumaa kwenye Msikiti wa al Aqsa na maeneo yake ya karibu

 

Sala ya Idul Fitr ilisaliwa pia jana Jumatano katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan ambapo Waislamu wa Palestina wameshiriki kwa maelfu kwenye Sala hiyo ndani na nje ya Msikiti wa al Aqsa ambao ni Kibla cha Kwanza cha Waislamu. 

Idara ya Wakfu wa Kiislamu na Masuala ya Msikiti wa al Aqsa katika mji wa Baytul Muqaddas imetangaza kuwa, karibu Wapalestina 60,000 wameshiriki kwenye Sala ya Idul Fitr ndani na nje ya Msikiti huo mtakatifu.

Taarifa ya idara hiyo imeongeza kuwa, licha ya wanajeshi makatili wa Israel kuweka vizuizi vingi na vikali, lakini maelfu ya Wapalestina wamehakikisha wanafika kwenye Msikiti wa al Aqsa na kutekeleza ibada ya Sala ya Idul Fitri ambayo ni katika sunna zilizotiliwa mkazo mno na dini tukufu ya Kiislamu.

Tags