Ismail Haniya: Ninamshukuru Allah kwa heshima hii aliyotupa ya kufa shahidi wanangu watatu na wajukuu zangu
Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS amethibitisha habari ya kuuawa shahidi watoto na wajukuu zake katika shambulio la kinyama la utawala wa Kizayuni na akasema: "kwa machungu haya na kwa damu hii tunajenga matumaini, mustakbali na uhuru wa watu wetu, piganio letu na taifa letu".
Katika taarifa aliyotoa kupitia televisheni, Haniya amesisitiza kwa kusema: "wakaliaji ardhi kwa mabavu wanadhani kwamba kwa kuwalenga watoto wa viongozi, watavunja azma ya watu wetu, lakini umwagaji damu huu utaimarisha tu uthabiti wetu katika misingi yetu na kushikamana kwetu na ardhi yetu."
Kiongozi wa Hamas ameongezea kwa kusema: “wanangu walibaki Ghaza na hawakuondoka katika eneo hilo; kama ilivyo kwa watoto wote, watu wetu wanalipa gharama kubwa katika damu ya watoto wao, na mimi ni mmoja wao.”
Haniya ameuhutubu utawala wa Kizayuni kwa msisitizo akisema: "tunaiambia Israel: kile ambacho hamjaweza kukipata kwa kufanya uharibifu, mauaji ya halaiki na uangamizaji, hamtakipata kwenye meza ya mazungumzo".../