Apr 28, 2024 11:53 UTC
  • Viongozi wa makundi ya Palestina wakutana Istanbul, Uturuki kujadili yanayojiri Ghaza

Viongozi wa Harakati za Hamas, Jihadul-Islami na Vuguvugu la Wananchi la Ukombozi wa Palestina wamekutana kujadili yanayojiri kwenye medani za mapambano na za kisiasa za Palestina na vita katika Ukanda wa Ghaza.

Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS imetangaza katika taarifa kwamba, kikao cha viongozi wa makundi ya Palestina cha kujadili matukio yanayoendelea kujiri kwenye uwanja wa mapambano na uga wa kisiasa katika Ukanda wa Ghaza kimefanyika mjini Istanbul, Uturuki kwa kuhudhuriwa na Ismail Haniya, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas, Muhammad Al-Hindi, Naibu Katibu Mkuu wa Harakati ya Jihadul-Islami, Jamil Mazher, Naibu Katibu Mkuu wa Vuguvugu la Wananchi la Ukombozi wa Palestina na viongozi wengine wa makundi hayo.
 
Taarifa ya Hamas imeeleza kuwa, waliohudhuria kikao hicho cha mjini Istanbul wamepongeza istikama na irada thabiti ya wananchi wa Palestina na kutangaza kuwa, taifa la Palestina limeuthibitishia ulimwengu kwamba kamwe halitasambaratika na wala halitashindwa licha ya mauaji ya kimbari aliyoyaanzisha adui.

Viongozi wa makundi ya Wapalestina wamezungumzia pia juhudi zinazofanywa ili kusimamisha vita, kuondoka haraka na kikamilifu maghasibu wa Kizayuni huko Ghaza, kuachiliwa huru wafungwa wa Kipalestina, njia zinazowezekana kufanywa ili kupunguza mateso na matatizo ya watu wa ardhi hiyo na kuimarishwa uthabiti na isitikama ya ndani mbele ya utumiaji mabavu na ubaguzi wa rangi wa wavamizi wa Kizayuni.

 
Halikadhalika, viongozi wa makundi ya Palestina wamesisitiza ulazima wa kuimarishwa harakati za kitaifa na kwenye medani ya vita ili kuzima njama za utawala unaoikalia Quds kwa mabavu na kuhakikisha malengo ya taifa la Palestina na piganio lake la uhuru, kujitawala na kurejea kwenye ardhi za asili yanafikiwa.../