Baraza Kuu la UN laimarisha haki za taifa la Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/world-i111628-baraza_kuu_la_un_laimarisha_haki_za_taifa_la_palestina
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa -UNGA limepitisha azimio  la kuongezea taifa la Palestina haki ndani ya Baraza hilo, sawa na nchi nyingine 193 wanachama. Pamoja na hayo Palestina bado haitakuwa na haki ya kupiga kura ndani ya chombo hicho cha ngazi ya juu cha maamuzi cha Umoja wa Mataifa.
(last modified 2024-05-11T01:21:09+00:00 )
May 11, 2024 01:21 UTC
  • Baraza Kuu la UN laimarisha haki za taifa la Palestina

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa -UNGA limepitisha azimio  la kuongezea taifa la Palestina haki ndani ya Baraza hilo, sawa na nchi nyingine 193 wanachama. Pamoja na hayo Palestina bado haitakuwa na haki ya kupiga kura ndani ya chombo hicho cha ngazi ya juu cha maamuzi cha Umoja wa Mataifa.

Azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu Kuandikishwa kwa Wanachama wapya katika Umoja wa Mataifa limesema:  “Baraza Kuu linaamua kuwa Taifa la Palestina lina sifa za kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa kwa mujibu wa kifungu cha 4 cha Chata ya UN na hivyo basi linapaswa kukubaliwa uanachama wa Umoja wa Mataifa. Kwa hiyo linapendekeza kwamba Baraza la Usalama liangalie upya suala hilo kwa upendeleo, kwa kuzingatia uamuzi huu na maoni ya ushauri ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki yaliyotolewa tarehe 28 Mei 1948, na kwa kuzingatia kikamilifu Ibara ya 4 ya Chata ya UN."

Azimio hilo lilipitishwa kwa kura 143 za kuunga mkono, 9 zinazopinga, na 25 za nchi ambazo zimejizuia kupiga kura.

Baraza kuu halitatoa hadhi ya uanachama kamili kwa Palestina kwa kuwa suala hilo linahitaji mapendekezo kutoka kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Tayari Baraza Kuu limeamua kwamba Palestina ina sifa za kupata hadhi hiyo na limependekeza kwamba Baraza la Usalama “liangalie upya suala hilo kwa upendeleo”.

Mwezi uliopita. Marekani ambayo ni muungaji mkono mkuu wa utawala wa kikoloni wa Israel kwa mara nyingine ilitumia kura ya turufu (veto) na kuzuia kupasishwa uanachama kamili wa Palestina ndani ya Umoja wa Mataifa.

Suala la kuipa uanachama Palestina katika Umoja wa Mataifa ni jinamizi kwa Tel Aviv na kwa msingi huo utawala wa Kizayuni na muungaji mkono wake mkuu Marekani zimekuwa zikipinga vikali Palestina kupewa unachama kamili katika UN.